1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Matumaini mapya ya mazungumzo Sudan

Angela Mdungu
29 Aprili 2023

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Volker Perthes amesema leo kuwa, pande zinazohasimiana kwenye mzozo unaoendelea nchini humo zimekubali kuwa, machafuko yaliyozuka wiki mbili zilizopita hayapaswi kuendelea

Sudan | Kämpfe in Khartoum
Picha: AFP/Getty Images

Hatua hiyo imeleta matumaini japo kidogo hata wakati mapambano yakiendelea. Perthes amesema pande hizo mbili hasimu ziliteua wawakilishi kwa ajili ya mazungumzo yaliyopendekezwa kufanyika Jeddah nchini Saudi Arabia au Juba, huko Sudan Kusini.

 Hata hivyo ameongeza kuwa, swali kubwa ni iwapo wawakilishi hao watafanikiwa kufika na kukaa kwenye moja ya mazungumzo. Mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa hajaainisha ikiwa kuna muda maalumu uliotengwa kwa ajili ya mazungumzo hayo.

Soma zaidi:Milio ya risasi inaendelea kusikika nchini Sudan licha ya kauli ya kusitisha mapigano

Matarajio ya mazungumzo kati ya viongozi wa pande zinazotofautiana hadi sasa yamekuwa madogo. Ijumaa, kiongozi wa jeshi rasmi la serikali, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan katika mahojiano alisema kamwe hatokaa chini na kiongozi wa wanajeshi wa kikosi maalumu cha RSF Mohamed Hamdan Dagalo.

Jenerali Mohamed Hamdan DagaloPicha: MOHAMED NURELDIN ABDALLAH/REUTERS

Kwa upande wake Dagalo alieleza kuwa atakuwa tayari kuzungumza ikiwa jeshi litasitisha uhasama.  Mamia ya watu wameuwawa tangu Aprili 15 kutokana na mzozo wa kuwania madaraka kati ya pande hizo mbili

Soma zaidi:Sudan: Makubaliano ya usitishwaji mapigano kufikia tamati

Perthes alieleza kuwa aliliambia baraza la usalama kuwa pande zote mbili zilizo kwenye mzozo zilidhani zitashinda, alisema pia hata hivyo mitazamo yao imeanza kubadilika. Alisema, "Wote wanadhani watashinda, lakini kwa kiasi Fulani wanatoa nafasi ya kufanyika kwa majadiliano, awali neno  majadiliano au mazungumzo halikuwa na nafasi”

Jenerali Abdel-Fattah BurhaniPicha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Aliendelea kueleza kuwa, "Wakati tayari pande hizo zikiwa zimeshatoa kauli kuwa upande wa pili ni sharti ujisalimishe au uchague kufa, sasa wanasema pia kuwa wanakubali walau kufikiria kuwa na mazungumzo”.

Mapigano yanaendelea licha ya matumaini ya majadiliano

Pamoja na hayo, jeshi rasmi limekuwa likifanya mashambulizi ya anga kila siku  na limesema limeendelea kudhibiti maeneo muhimu. Wakaazi wameeleza kwamba kwa upande wao RSF wameendelea kuuwa na nguvu zaidi katika mapambano ya ardhini mjini Khartoum

Mapigano hayo yanayoendelea, yamesababisha uharibifu wa miundombinu ya umeme, maji na mawasiliano huku matukio ya uporaji yakiharibu makazi ya wat una biashara. Maelfu ya raia wamekimbilia kwenye miji mingine na hata katika nchi Jirani

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW