1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya kuangamiza ufukara Afrika yachomoza

8 Februari 2019

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yamebaini katika utafiti wao kwamba fedha zinazotengwa kwa ajili ya watoto barani Afrika zimesaidia kuleta matokeo mazuri katika kutokomeza umasikini.

NGO Little Dresses for Africa
Picha: LDFA Portugal

Utafiti wa pamoja wa shirika la kimataifa la ajira ILO na shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto ulimwenguni UNICEF  unaonyesha kwamba fedha zinazotumiwa kwa ajili ya huduma za kimsingi kwa watoto, zimekuwa na matokeo chanya katika kuukabili ufukara, usalama wa upatikanaji wa chakula, afya na elimu hivyo basi kusaidia watoto kustawi na kupunguza kukua kwa viwango vya ufukara.

Umoja wa mataifa unasema fedha hizo za misaada kwa ajili ya ustawi wa watoto barani Afrika zina uwezo mkubwa sana wa kupunguza viwango vya umaskini duniani. Utafiti huo unaeleza kwamba sio swala la fedha tu linaloweza kufanikisha kupungua kwa viwango vya ufukara ila sera pana zinahitajika ikiwemo mpango wa chakula kwa wanafunzi shuleni.

Takwimu zinaonyesha kufikia mwaka 2030 asilimia 90 ya watoto katika nchi za Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara watakuwa wanaishi katika umasikini. Nchi 40 kati ya 48 barani Afrika zina mipango fulani ya uhamishaji fedha kwa watoto ila kiwango wanachopewa watoto hao ni cha chini mno na asilimia 13.1 pekee ndio wanaopokea fedha hizo.

Watoto hawa wa wakimbizi wa Congo nchini Angola wanahitaji msaada wa kifedha kuwaepusha na mzunguko wa umasikini barani AfrikaPicha: UNICEF/N. Wieland

Mkuu wa kitengo cha kupambana na umasikini katika shirika la UNICEF, David Stewart, amewaambia waandishi habari mipango hiyo yote si mikubwa lakini umekuwa ufanisi na ukuaji muhimu katika eneo hilo na ukuaji unafanyika haraka. 

"Ushahidi unaonyesha dhahiri shahiri kwamba kutokana na tathmini kutoka Afrika, Amerika Kusini na Ulaya kuna ufanisi mkubwa kwa maisha ya watoto. Kwa watoto wengi, umasikini ndio unawazuia kwenda shule, kukosa afya na kuosa lishe bora. Na inaonyesha kwamba ukitoa fedha kwa watoto hawa kunapatikana mabadiliko makubwa sana mazuri kwa afya zao na elimu, jambo linalobadilisha mustakabali wao na nafasi nzuri za maisha baadaye na bila shaka mabadiliko makubwa katika jamii," alisema Stewart.

Asilimia 42.9 katika mataifa ya Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara ni watoto, mataifa hayo yanatenga asilimia 0.7 pekee katika pato la taifa kwa mwaka kwa ajili ya watoto.

Afrika Kusini mfano wa kuigwa

Mkuu wa maswala ya kijamii katika shirika la ILO, Isabel Ortiz, amesema taifa la Afrika Kusini limepiga hatua kubwa japo haliwashughulikii watoto wote huku Ghana ikielekeza ruzuku za mafuta kwa watoto nayo Zambia ikiongeza ushuru wa madini, haya yote yakidhihirisha serikali hizo zinaweza iwapo zitakuwa na nia. 

Makao makuu ya shirika la ILO Geneva, UswisiPicha: picture-alliance/maxppp/V. Isore

Isabel amesema haitoshi kwa serikali za mataifa ya Afrika kusema hazina bajeti wa ajili ya watoto. "Asilimia 35 ya watoto wako katika mipango mbali mbali ya ulinzi wa kijamii. Hakika hiki ni kiwango cha kusikitisha kwa sababu ina maana thuluthi mbili za watoto duniani hawapati huduma zozote za msaada. Hao ni watoto bilioni 1.3 ambao ni wengi. Mipango ya usaidizi inaweza kupunguza umasikini na idadi ya watoto walioko katika umasikini mara moja iwapo mipango hii itakuwa ya kutosha. Kwa hivyo mataifa yanahitajika kuongeza juhudi zaidi katika kuboresha huduma za kimsingi kwa watoto na makundi mengine."

Kiasi kikubwa cha watoto ulimwenguni wanaishi katika umaskini kwa wastani kwa siku hutumia chini ya dola moja, nusu yao wakiwa barani Afrika ambapo kuna udhaifu katika mifumo ya utoaji wa huduma za kijamii.

Kiasi cha thuluthi moja ya watoto ulimwenguni wako katika mpango maalum wa kijamii huku asilimia 88 wakiwa ni watoto katika bara la Ulaya na Asia ya Kati na asilimia 16 barani Afrika.

Mashirika ya ILO na UNICEF pia yametoa tahadhari ya kurudi kwa ufukara Ulaya kutokana na serikali hizo kupunguza mafao ya watoto kwa sababu ya hatua ya serikali hizo kufunga mkaja.

Mwandishi: Faiz Musa/APE

Mhariri: Josphat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW