Matumaini ya kufufua mazungumzo ya nyuklia yazidi kudidimia
26 Machi 2021Wakati ambapo Iran inakaribia kuingia kwenye kampeni za uchaguzi wa rais, kiongozi mkuu wa nchi hiyo ameshikamana na msimamo mgumu kabla ya nchi yake kurudi kwenye mazungumzo hayo ingawa Marekani na washirika wake wa Magharibi bado wana matumaini kuhusiana na mazungumzo hayo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran. Rais wa Marekani aliyeondoka Donald Trump aliiondoa nchi yake kwenye makubaliano hayo.
Utawala wa Rais Joe Biden umesema upo tayari kuzungumza na Iran juu ya mataifa hayo mawili kuanza tena kufuata hatua za makubaliano hayo, ambayo yaliwezesha kufutwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran ambapo Iran nayo ilihitajika kupunguza viwango katika uzalishaji wa madini ya Urani ili kuizuia nchi hiyo kuwa na uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia. Iran mara zote imesisitiza kwamba haitaki na wala haina nia ya kuwa na silaha za nyuklia.
Shida kubwa iliyopo ni kwamba kati ya nchi hizi mbili hakuna inayotaka kuchukua hatua kwanza. Tehran inasema Washington lazima iiondolee vikwazo vilivyowekwa na Donald Trump, mtangulizi wa Joe Biden, aliyeamuru kuwekwa vikwazo hivyo mara baada ya kuiondoa Marekani kwenye makubaliano hayo mnamo mwaka 2018, na kwa upande wake Washington inasema Tehran lazima kwanza ianze tena kufuata makubaliano hayo ambayo imekuwa ikiendelea kuyakiuka tangu mwaka 2019.
Wanadiplomasia wawili wa magharibi na maafisa wawili wa Iran wamesema wizara za mambo ya nje za nchi hizo ziliandaa mapendekezo na hatua kwa hatua juu ya vipi pande mbili hizo zingerejea katika mazungumzo kwa kuzingatia makubaliano yaliyopo. Kwenye mpango huo ilipendekezwa Iran iache kuzalisha madini ya Urani kwa asilimia 20 na Marekani nayo ilitakiwa kuziachilia dola bilioni 15 fedha za Iran zinazozuiwa nje ya nchi hiyo. Mapendekezo hayo yalikataliwa na Iran ikisisitiza kuwa hayangeweza kuhakikisha unafuu wa vikwazo dhidi ya nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Javad Zarif amesema iwapo hakutapatikana maendeleo juu jambo hilo hivi karibuni basi diplomasia itakwama kwa miezi kadhaa kutokana na uchaguzi wa rais wa Iran uliopangwa kufanyika tarehe 18 Juni.
Sera ya nyuklia ya Iran inamtegemea kiongozi wa kidini Ali Khamenei, ambaye hayumo kwenye mchakato wa kugombea kwenye uchaguzi huo lakini, kutokuelewana kati ya Marekani na Iran kunaweza kuwashawishi wapiga kura na hatimae kusababisha kupungua idadi ya watakaojitokeza kupiga kura na hivyo kuwaimarisha wale ambao wanaamini katika ulazima wa utawala wa Iran kuanzisha hatua za kulegeza misimamo mikali kwenye sera yake hiyo ya nyuklia.
Mwanadiplomasia mmoja mwandamizi wa Ulaya amesema mambo yamekwama na wakati unayoyoma kabla ya uchaguzi wa rais nchini Iran. Amesema Ufaransa, Uingereza na Ujerumani washirika wa Ulaya kwenye makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, bado wanafanya kila linalowezekana kupata mafanikio.
Mmoja wa wanadiplomasia wa magharibi naye amesema tathmini ya nchi za Ulaya ni kwamba kiongozi mkuu wa Iran Khamenei, hatarudi nyuma katika msimamo wake kwa sasa, ingawa Iran inaweza kutoa pendekezo lake kabla ya mwezi Juni, na kwamba huenda Marekani na washirika wake wa Ulaya nao wakakataa kulikubali pendekezo hilo la Iran.
Mchambuzi wa kundi la Eurasia, Henry Rome, amesema uwezekano wa kufanyika mazungumzo upo lakini sio kabla ya uchaguzi wa rais wa nchini Iran uliopangwa kufanyika mwezi Juni.
Chanzo:/RTRE