1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah

1 Novemba 2024

Irael imeushambulia Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu ambapo watu watatu wameuawa. Na Lebanon imesema kuna matumaini ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah

Mashambulizi ya Israel kusini mwa Beirut
Mashambulizi ya Israel kusini mwa BeirutPicha: Marwan Naamani/ZUMA/picture alliance

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina Wapalestina wawili wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel na wa tatu ameuawa kutokana na kupigwa risasi katika kambi ya wakimbizi ya Nur Shams ambayo mapambano yamekuwa yakiendelea mara kwa mara.

Jeshi la Israel kwa upande wake limesema vikosi vyake viliwalenga wapiganaji kwenye kambi hiyo ya wakimbizi na limefanikiwa kumuua mpiganaji mmoja wa kundi la Hamas ambaye wanasema alihusika katika kupanga mashambulizi dhidi ya raia Waisraeli.

Soma Pia: Misri yapendekeza kusitishwa mapigano na kuachiliwa mateka  

Wakati hayo yakiendela huko nchini Lebanon, Waziri Mkuu wa muda Najib Mikati amesema ana matumaini juu ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hezbollah katika muda usio mrefu.

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kwamba mjumbe maalum wa Marekani Amos Hochstein, atakwenda Israel leo Alhamisi kwa mazungumzo akiwa anaandamana na Brett McGurk, ambaye ni Mratibu wa Ikulu ya Marekani anayeshughulikia maswala ya eneo la Mashariki ya Kati.

Uharibifu wa majengo katika mashambulizi ya Israel kusini mwa BeirutPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Waziri mkuu wa Lebanon Najib Mikati ameelezea matumaini yake kuhusu kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano wakati shirika la utangazaji la Israel likiwa limechapisha rasimu ya awali ya makubaliano hayo ya kusitisha mapigano kwa siku 60.

Kiongozi mpya wa Hezbollah Naim Qassem amesema kundi lake linaloungwa mkono na Iran liko tayari kwa mazungumzo ya kumaliza vita na Israeli lakini kwa masharti.

Soma Pia: Israel yashambulia Gaza, Lebanon na Syria

Israel na kundi la Hezbollah la nchini Lebanon wamekuwa wakipigana kwa muda wa mwaka mmoja sambamba na vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Mzozo nchini Lebanon umeongezeka kwa kasi katika muda wa wiki tano zilizopita, watu wapatao 2,800 wakiripotiwa na wizara ya afya ya Lebanon kuuawa katika kipindi hicho.

Wizara ya Afya ya Lebanon pia imesema watu 19 waliuawa siku ya Jumatano katika mashambulio ya anga ya Israel kwenye mji wa Baalbek ulio mashariki mwa Lebanon.

Vyanzo: DPA/RTRE/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi