1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya upatikanaji chanjo ya corona yaongezeka

16 Novemba 2020

Matumaini ya kupatikana chanjo ya virusi vya corona yanazidi kuongezeka baada ya kampuni ya dawa ya Moderna Inc kusema chanjo yake imeonyesha mafanikio kwa asilimia 94.5 katika kuzuia maambukizi ya COVID-19.

Coronavirus Impfstoff Symbolbild
Picha: picture alliance/dpa

Matumaini ya kupatikana chanjo ya virusi vya corona yanazidi kuongezeka baada ya kampuni ya dawa ya Moderna Inc kusema kwamba chanjo yake imeonyesha mafanikio kwa asilimia 94.5 katika kuzuia maambukizi ya COVID-19. Hayo yanatokea wakati kansela wa Ujerumani Angela Merkel akitaraji kukutana na mawaziri wakuu wa majimbo 16 ili kutathmini athari za kufungwa kwa baadhi ya shughuli nchini humo kufuatia kuongezeka kwa maambukizi. Lilian Mtono anaarifu.

Moderna imesema chanjo yake imeonyesha mafanikio kwa asilimia 94.5, kufuatia taarifa za awali kutoka kwenye kampuni hiyo baada ya utafiti unaoendelea. Wiki moja iliyopita, mshindani wake Pfizer Inc zote za nchini Marekani ilitangaza chanjo yake ya COVID-19 kwamba nayo imeonyesha mafanikio makubwa. Taarifa hizo zimeyakutanisha makampuni hayo kwa pamoja katika mchakato wa kusaka kibali cha matumizi ya dharura ya chanjo hizo nchini Marekani.

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: bundesregierung.de

Dokta Stephen Hoge, rais wa kampuni ya Moderna ameikaribisha taarifa hiyo na kusema ni hatua muhimu, akisema kuwepo na matokeo ya kufanana kutoka kwenye makampuni mawili tofauti ndicho kitu kinachowahakikishia kwamba chanjo hiyo inaleta matumaini makubwa.

Ameliambia shirika la habari la AP kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba chanjo hiyo italizuia janga hilo na kuna matarajio kwamba hatimaye Marekani itarudia maisha ya kawaida.

Mtaalamu wa ngazi za juu kabisa wa magonjwa ya kuambukiza nchini humo Dr. Anthony Fauci amewaambia waandishi wa habari kwa njia ya simu kwamba chanjo hiyo imeleta mwangaza mkubwa. Fauci hata hivyo amewaomba Wamarekani kutobweteka na taarifa hizo akiwataka kuendelea kujikinga.
Huku hayo yakiendelea, nchini Ujerumani Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pamoja na mawaziri wakuu wa majimbo yote 16 ya Ujerumani wanataraji kufanya tathmini ya athari za hatua ya kusimamisha baadhi ya shughuli iliyodumu kwa takriban wiki mbili, katika harakati za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona, huku kukitarajiwa kutangazwa vizuizi vipya.

Ujerumani ilichukua hatua ya kufunga baadhi ya shughuli, mwanzoni mwa mwezi Novemba iliyohusisha kufunga mikahawa na majumba ya makumbusho lakini tofauti na awali haikuzifunga shule na maduka ya vyakula, kufuatia kuongezeka kwa kasi kwa virusi vya corona mwezi Oktoba.

Ongezeko la maambukizi mapya imepungua tangu kuchukuliwa kwa hatua hiyo, lakini siku ya Ijumaa Ujerumani ilirekodi visa 23,542, idadi ya juu kabisa ya maambukizi mapya. Siku ya Jumatatu, taasisi ya kupambana na magonjwa imerekodi visa vipya 10,824, lakini idadi hiyo mara zote huwa ni ya chini mwanzoni mwa wiki kwa kuwa hufanyika vipimo vichache mwishoni mwa wiki na pengine taarifa kuchelewa kufika kituoni hapo.

Picha: picture alliance / NurPhoto

Kansela Merkel pamoja na magavana hao 16 pia wanataraji kuanzisha vizuizi vipya, ambavyo ni pamoja na kuvaa barakoa shuleni pamoja na vizuizi vikali kuhusu mikusanyiko ya nyumbani ili kukabiliana na wimbi la pili kabla ya sikukuu za Christmas.

Muswada kuhusiana na vizuizi hivyo ulioonwa na shirika la habari la Reuters umesema watu wataombwa kujizuia kabisa na mikusanyiko ya sherehe katika kipindi cha wiki zijazo.

Kansela Merkel amenukuliwa na shirika la habari la Ujerumani la DPA akiwaambia wafuasi wa chama chake cha Christian Democratic Union, CDU kwamba idadi ya maambukizi inapungua, lakini taratibu mno.

Kulingana na muswada huo, wataalamu wa Ujerumani wanatarajia kulikabili janga hilo baada ya majira ya baridi hasa kwa kuwa kasi yake ya maambukizi imeshuka kutokana na hali ya joto na pengine kuanza kutolewa chanjo.

Kulingana na muswada huo ambao hata hivyo unaweza kubadilika kwa kuzingatia mazungumzo kati ya serikali ya shirikisho na serikali za majimbo 16, mikusanyiko binafsi kwenye maeneo ya umma huenda ikafanyika tu kwa watu wanaotoka nyumba moja na wengine wawili kutoka kwenye nyumba nyingine, tofauti na awali ambapo idadi ya juu kabisa ilikuwa watu 10 kutoka familia mbili.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW