1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Matumaini ya usuluhishi Niger kabla ya mkutano wa ECOWAS

8 Agosti 2023

Nchi za Afrika magharibi pamoja na mataifa mengine duniani bado yanatumai pana fursa ya usuluhishi kwa njia ya mazungumzo na wanajeshi waliotwaa mamlaka nchini Niger.

Niger, Niamey | Jen. Abdourahmane Tchiani
Jen. Abdourahmane Tchiani kiongozi wa kijeshi wa NigerPicha: Balima Boureima/AA/picture alliance

Nchi za Afrika magharibi pamoja na mataifa mengine duniani bado yanatumai pana fursa ya usuluhishi kwa njia ya mazungumzo na wanajeshi waliotwaa mamlaka nchini Niger kabla ya kufanyika kikao cha viongozi wa nchi za jumuiya ya kiuchumi ya ECOWAS hapo siku ya  Alhamisi kuujadili mgogoro huo. Wanajeshi walioipindua serikali mwezi uliopita wameazimia kupinga mashinikizo yoyote kutoka nje ya kuwataka wamrejeshe madarakani rais Mohamed Bazoum waliyemwondoa madarakani.

Jumuiya ya ECOWAS imeweka vikwazo dhidi ya Niger na nchi za magharibi zimesimamisha misaada. Wakati huo huo aliyekuwa naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Victoria Nuland amefanya mazungumzo na wanajeshi waliotwaa mamlaka. Nuland amesema mazungumzo yalikuwa ya dhati lakini magumu. Ameeleza kuwa wanajeshi hao wameyakataa mapendekezo ya Marekani juu ya kurejesha utaratibu wa kidemokrasia nchini NIger.