Matumaini yachomoza Brussels
14 Desemba 2012Baada ya zaidi ya masaa manane ya majadiliano, viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya wameahidi kusonga mbele na juhudi zao za kubuni mkakati wa kukabiliana na matatizo yanayozikaba benki ingawa haikuwa dhahiri lini mkakati huo utakamilika.
"Tumekubaliana kuhusu muongozo wa siku za mbele wa umoja wa sarafu," amesema kansela wa Ujerumani, Angela Merkel mbele ya waandishi habari bila ya kutoa maelezo zaidi..
Wameanzisha pia mijadala juu ya jinsi nchi zinavyoweza kufuata malengo yaliyowekwa ya kiuchumi na kubuni "fuko la mshikamano ili kuyasaidia mataifa yanayosumbuliwa na migogoro ya fedha.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wametoa mwito makubaliano yafikiwe hadi mwezi Juni mwakani. Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, anashauri awamu ya kwanza ya mkakati huo wa kusimamia shughuli za benki ianze mwishoni mwa mwaka 2013 na ya pili mapema mwaka 2014. Lengo ni kuona mkakati huo unapitishwa na bunge la sasa la Ulaya.
Spika wa bunge la Ulaya, Martin Schulz, ambaye alishiriki hapo awali mazungumzoni anasema:"Huu ni msingi wa majadiliano ya miezi kadhaa kuhusu wapi, lini na vipi madeni ya mataifa wanachama yanaweza kudhaminiwa kwa pamoja . Naamini huu ndio msingi ambao tumekuwa tukiushughulikia tangu muda mrefu sasa."
Kansela Merkel amefafanua mkakati mzima jinsi utakavyofanya kazi katika daraja ya Ulaya na akasisitiza kwamba "haupaswi kuangukia mabegani mwa walipa kodi."
Mkutano huo wa siku mbili wa viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya, wa sita na wa mwisho kwa mwaka huu wa 2012, ulilenga tangu mwanzo kusaka njia bora za kupambana na mgogoro wa kiuchumi na kurekebisha matatizo yaliyosababishwa na miaka mitatu ya mgogoro wa madeni.
Mkutano wa viongozi umefanyika saa chache baada ya mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya kufikia makubaliano kuhusu "umoja wa benki" kwa kukubaliana kwamba benki kuu ya Ulaya ndiyo itakayosimamia shughuli za benki ya kanda ya Euro.
Uamuzi huo pamoja na maamuzi mengine yaliyofikiwa na mawaziri wa fedha wa kanda ya Euro kuipatia Ugiriki msaada mwengine wa Euro bilioni 50 ndio matokeo ya maana yaliyofikiwa hadi wakati huu. Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya unaendelea hii leo mjini Brussels.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo