Matumaini yazidi kuimarika, Yemen
17 Aprili 2020Hali ya matumaini imezidi kuimarika katika juhudi za kumaliza mzozo wa kivita nchini Yemen. Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya nchi hiyo Martin Griffiths ameliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mazungumzo baina ya serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa na waasi wa Kihouthi yamepiga hatua kubwa.
Mjumbe huyo amesema kitisho cha janga la virusi vya corona kimeweka msukumo katika mchakato wa kutafuta amani nchini Yemen, na kuongeza kuwa anatarajia kwamba pande zinazohasimiana zitaafiki mpango wa kudumu wa usitishaji mapigano na kuanza mazungumzo mnamo siku chache zijazo.
Martin Griffiths ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa anaamini kwamba wanakaribia muafaka wa kusitishwa kwa mapigano katika maeneo yote ya Yemen, kati ya vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia, na waasi wa Kihouthi ambao ni washirika wa Iran.
''Mazungumzo tuliyoyafanya na pande hizo mbili, na mashauriano kati yetu na ushirika wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na wadau wengine wa kimataifa yanaendelea ni ya kina na ni yenye tija. Naweza kutangaza kwamba tumepiga hatua nzuri kabisa kuelekea muafaka juu ya mapendekezo ya kusitisha mapigano katika maeneo yote ya Yemen.'' alisema Griffiths.
Griffiths amesema ujumbe anaouongoza unafanya kila liwezekanalo kujaribu kupunguza tofauti zinazosalia baina ya pande hasimu kabla ya kuzileta kwenye meza moja ya mazungumzo, ambako makubaliano yatafikiwa na kisha kuchapishwa rasmi.
Kuzuka kwa janga la virusi vya corona ambalo kwa mara ya kwanza lilithibitishwa nchini Yemen mapema mwezi huu, kulitishia kuzidisha maafa kwa watu wa taifa hilo maskini zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu, ambalo linakumbwa na mzozo mbaya wa kivita tangu mwaka 2014.
Tayari watu wapatao 100,000 wamekwishapoteza maisha katika vita hivyo, na mamilioni wengine wanapambana na athari kali za kibinadamu zinazosababishwa na mzozo huo. Upungufu mkubwa wa chakula na madawa umeipeleka nchi hiyo kwenye ukingo wa baa la njaa.
Soma Zaidi:Yemen: Miaka mitano ya vita visivyo na dalili ya kuisha
Ijumaa iliyopita, mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa aliwasilisha kwa pande zinazohasimiana nchini Yemen, mapendekezo mapya kuhusu usitishaji mapigano kote nchini, kuanza duru mpya ya mazungumzo, na mkakati wa kuufufua uchumi na kupunguza madhila kwa umma wa Yemen.
Amesema hakuna muda bora kuliko wa sasa kwa pande hizo kunyamazisha silaha na kuumaliza mzozo kwa njia za kisiasa mzozo unaoisambaratisha nchi yao.
Licha ya matumaini hayo lakini, msemaji wa upande wa Wahouthi Mohammed Abdel Salah amesema mapendekezo hayo mapya yamepuuza sharti lao muhimu, ambalo ni kuitaka Saudi Arabia iondoe mzingiro wa angani na baharini, ambao maafisa wa mashirika ya msaada wanaushutumu kuzidisha madhila kwa raia wenye mahitaji ya dharura.
Mashirika: ape, dpae.