1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nishati ya visukuku kuwagawa viongozi COP28

Sylvia Mwehozi
1 Desemba 2023

Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan, ambaye nchi yake ndiyo mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa mazingira wa COP28, ametangaza kuanzishwa mfuko wa mazingira wa Dola bilioni 30.

COP28 Dubai
Viongozi wa dunia wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa COP28.Picha: Peter Dejong/AP/dpa/picture alliance

Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan, ambaye nchi yake ndiyo mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa mazingira wa COP28, ametangaza hii leo kuanzishwa kwa mfuko wa kimazingira wa Dola bilioni 30 unaokusudia kuvutia uwekezaji zaidi kufikia mwisho wa muongo. COP28 yazindua mfuko wa hasara na uharibifu wa tabianchi

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa COP28, mfuko huo uliopachikwa jina la ALTÉRRA utatenga kiasi cha dola bilioni 25 kuelekea mikakati ya mazingira na dola bilioni 5 zitaelekezwa kwenye kuhamisha uwekezaji kwenye mataifa yenye kiwango duni cha maendeleo ya kiuchumi na kiviwanda.

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa mfuko huo utaelekeza masoko binafsi katika uwekezaji wa mazingira na kuzingatia kubadilisha masoko yanayoibukia na chumi zinazoendelea, ambako uwekezaji wa kijadi umekosekana kutokana na hatari kubwa zilizopo.

Katika siku ya pili ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliwahimiza viongozi wa ulimwengu kujipanga kwa ajili ya mustakabali wa baadae bila ya matumizi ya mafuta ya visukuku akiongeza kuwa hakuna namna yoyote ulimwengu utaweza kukabiliana na ongezeko la joto duniani.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mkutano wa COP28Picha: DHA

Guterres ametoa kauli hiyo siku moja baada ya rais wa COP28 Sultan Ahmed al-Jaber kupendekeza kuendelea na matumizi ya mafuta ya visukuku. Mitizamo hiyo kinzani inatoa taswira juu ya suala lenye mgawanyiko linalowakabili viongozi wa ulimwengu katika mkutano wa mwaka huu wa kilele unaofanyika huko Dubai. 

Mfalme Charles ahimiza ukarabati wa haraka wa mazingira

Kiongozi mwingine aliyezungumza ni Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen aliyetoa wito kwa viongozi wa dunia kuchukua "hatua madhubuti" za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuwalinda wale walioko hatarini zaidi.

"Katika mkutano huu wa COP tutaweka hatua madhubuti za kuwalinda raia walio hatarini zaidi ulimwenguni. Wanapitia mabadiliko ya tabia nchi, wanapata hasara na uharibifu na tutasimama upande wao. COP hii inahusu matamaini, inahusu malengo na inahusu ufadhili."

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva akizungumza katika COP28Picha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Kando na hayo, ni kwamba zaidi ya nchi 130 zimekubali kujumuisha chakula na kilimo katika mipango yao ya kitaifa ya mazingira katika hatua iliyopongezwa na waangalizi licha ya hofu juu ya ukimya wake kuhusu nishati itokanayo na mafuta ya visukuku.

Jumla ya nchi 134 zinazozalisha asilimia 70 ya chakula kinachotumika duniani kote zilitia saini tamko hilo, kwa mujibu wa wenyeji wa mkutano huo Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kwanini mikutano ya COP imekuwa mingi: Kuna haja gani kuandaa mikutano ya COP kila mwaka?

Katika hatua nyingine wajumbe wa Iran wamelazimika kuondoka katika mkutano huo kupinga uwepo wa wawakilishi wa Israel. Waziri wa nishati wa Iran Ali Akbar Mehrabian, alisema kuwa uwepo wa Israel katika mkutano huo ni "kinyume na malengo na miongozo ya mkutano huo," ndio maana wameamua kuondoka.

Viongozi wengine watatatoa hotuba zao mwishoni mwa juma.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW