1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji mengine Tana River

11 Septemba 2012

Watu wenye silaha kutoka jamii moja miongoni mwa mbili zinazohasimiana katika wilaya ya Tana iliyo mkoa wa Pwani wa Kenya wamewaua polisi watatu na kufanya mauaji mengine ikiwa ni mara ya tatu ndani ya siku tatu tu.

Nesi akimuhudumia muhanga wa mapigano ya Tana River.
Nesi akimuhudumia muhanga wa mapigano ya Tana River.Picha: Reuters

Tukio hilo limekuja siku moja tu baada ya kuzuka mauaji mengine ya watu 38 usiku wa kuamkia jana katika uhasama unaoendelea kati ya jamii za Pokomo na Orma.

Maafisa wanasema watu waliokuwa na silaha wamezichoama moto nyumba na kufyatua risasi ovyo katika eneo la Semikaro. Mbali na kuuwawa polisi hao watatu, watu wengine 6 pia walipoteza maisha yao.

Mashambulizi haya mapya yametokea masaa machache tu baada ya Rais wa Kenya Mwai Kibaki, kuamuru amri ya kutotoka nje kuanzia magharibi hadi alfajiri kufuatia mashambulizi ya hapo Jumatatu ambapo kiasi ya Wapokomo 300 walikivamia kijiji cha Kilelengwani na kuwashambulia Waorma ambapo watu 9 waliuawa.

Kibaki ameamuru pia kuongezwa kwa askari wa usalama katika eneo hilo. Akizungumzia juhudi zinazofanywa na Shirika la Msalaba Mwekundu kuwasaidia waathirika, msemaji wa Shirika hilo nchini Kenya, Abbas Gullet aliimbia DW kuwa wamepeleka magari ya kubebea wagonjwa, madaktari na madawa kwenye eneo hilo.

Zaidi ya Wakenya 200 wauawa

Msalaba Mwekundu wanasema kwamba zaidi ya Wakenya 200 waliuawa katika mapigano ya kikabila mwezi Januari. Bado watu wanaendelaea kukimbia Wilaya hiyo ya Tana River. Gullet alisema wengi wanakimbilia kwa jamaa na marafiki walioko maeneo mengine.

Wanakijiji wakiangalia mabaki ya nyumba zao baada ya kuchomwa moto.Picha: dapd

Ulipizaji kisasi kati ya jamii hizo mbili tayari umesababisha mauti ya watu 52 mwezi uliopita. Mashambulizi haya yanatoa kitisho kikubwa kwa Kenya ambayo inajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwezi Machi mwaka ujao, baada ya umwagaji damu uliotokea katika mapigano ya kikabila baada uchaguzi mkuu wa 2007, ambapo karibu watu 1,200 waliuawa na mamia kuyakimbia makaazi yao.

Wachambuzi wanasema tatizo kubwa panapohusika na mashambulizi ya Tana River ni silaha zinazoingia kutoka nchi jirani ya Somalia, wakisisitiza juu ya umuhimu wa serikali kuchukua hatua kuidhibiti hali hiyo, kama sehemu ya juhudi za kuituliza hali ya mambo na kurejesha usalama katika eneo hilo.

Mwandishi: Mohamed Abdul-rahman
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW