Mauaji nchini India watuhumiwa wapewa kifungo cha maisha
10 Juni 2019Mahakama pia ilitoa adhabu kwa polisi watatu ya kifungo cha miaka mitano kila mmoja kwa kosa la kuvuruga ushahidi. Mwili wa marehemu huyo aliyekuwa Mwislamu ulikutwa msituni karibu na mji wa Kathua mwaka uliopita ukiwa umekatwakatwa.
Watu hao watatu waliohukumiwa kifungo cha maisha ni Sanjhi Ram afisa wa serikali aiyestaafu ambaye pia ni msimamizi wa hekalu la Wahindu, mwingine ni Parvesh Kumar pamoja na afisa wa polisi, Deepak Khajuria. Walipatikana na hatia ya mauaji ya kudhamiria ubakaji na matumizi ya nguvu. Wakili wa watu walowasilisha mashtaka, Moobin Faruoqi Khan amesema atakata rufaa kwenye mahakamu kuu.
Kulingana na ushahidi uliotolewa, msichana huyo alitekwa nyara wakati alipowapeleka farasi kwa ajili ya malisho kwenye kijiji cha Jammu kilichopo katika eneo lenye idadi kubwa ya wahindu, mkasa huo ulitokea mwaka uliopita wa 2018. Marehemu alitiwa ganzi na kufungiwa ndani ya hekalu kwa muda wa siku tano.
Alibakwa mara kadhaa na kupigwa marungu hadi alikufa. Uchunguzi ulibainisha kwamba wahalifu walitenda kitendo Hicho ili kusababisha hofu miongoni mwa jamii ya watu wanao hamahama ya marehemu. Lengo lilikuwa kuwatisha ili waondoke kwenye sehemu yao.
Mshtakiwa mmoja miongoni mwa wanane aliachiwa kwa madai kwamba hajafikia umri wa kuhukumiwa lakini hata hivyo atafunguliwa kesi peke yake. Waendesha mashtaka wamesema wataingalia upya hukumu hiyo na kuamua iwapo watakata rufaa. Familia ya marehemu ambayo haikuhudhuria mahakamani ilitarajia adhabu ya kifo kwa waliomuua msichana huyo.
Mkasa wa mtoto huyo ulitifua wimbi la malalamiko na ghasia kwenye miji kadhaa ya India, ikiwa pamoja na mji mkuu New Delhi, Mumbai na Bangalore. Chama tawala cha Bharatiya Janata kilijitia dosari kutokana na wanachama wake wawili kuandamana kwa ajili ya kuwaunga mkono washtakiwa. Mikasa karibu 20,000 ya ubakaji iliripotiwa mnamo mwaka 2016 na kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2014 thuluthi moja ya waliobakwa walikuwa watoto.
Vyanzo:/DPAE/AFP