Mauaji ya mbunge wa Uingereza ni kisa cha kigaidi- polisi
16 Oktoba 2021Kulingana na polisi, matokeo ya awali ya uchunguzi wao yamebaini kile kinachoweza kuhusishwa na "motisha kutokana na msimamo mkali wa Kiislamu.”
Polisi imesema hayo inapochunguza kisa hicho cha pili tangu mwaka 2016 cha kuuawa kwa mwanasiasa wakati wa kukutana na wapiga kura tangu.
Amess, mwenye umri wa miaka 69 na mwanachama wa kihafidhina aliyeunga mkono Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya, alichomwa kisu usiku wa kuamkia Jumamosi akiwa kanisani akishauriana na watu wa êneo bunge lakem kijiji cha Leigh-on-Sea mji wa Essex, mashariki mwa London.
Uchunguzi dhidi ya kigaidi waendelea
Maafisa wa polisi wamemtia nguvuni mshukiwa mmoja mwenye umri wa miaka 25 kwa tuhuma ya kufanya mauaji, na vilevile wamekamata kisu.
Polisi ya Essex imesema maafisa wake walifika katika eneo la mkasa dakika chache baada ya ripoti hizo kuwafikia na kumpata Amess akiwa na majeraha kadhaa ya kuchomwa kisu.
"Hiki kilikuwa kisa kigumu, lakini maafisa wetu pamoja na wahudumu wa afya walifanya bidii kumuokoa Sir David,” amesema Ben-Julian Harrington, mkuu wa polisi wa Essex. "Kwa bahati mbaya akafa katika êneo hilo la mkasa.”
Soma pia: Mshambuliaji wa upinde na mshale aua watano Norway
Usiku wa kuamkia Jumamosi, misa ya ghafla kwa ajili ya marehemu iliandaliwa kwa Amess, baba wa watoto watano na ambaye alichaguliwa mwanzo kuingia bungeni mwaka 1983, huku wakituma rambirambi zikimiminika kutoka kwa wanasiasa na ulimwengu kwa jumla.
Mauaji ya Amess yaibua wasiwasi Uingereza
Vyombo vingi vya habari vya Uingereza vilinukuu duru ya habari iliyosema kwamba mshukiwa wa mauaji anaaminiwa kuwa raia wa Uingereza mwenye asili au urithi wa Kisomali.
"Uchunguzi ungali katika hatua za mwanzo na unaongozwa na wataalamu kutoka kamandi ya kupambana na ugaidi,” Ben-Julian Harrington amewaambia waandishi wa habari.
Kisa hicho kimezusha hofu kubwa nchini Uingereza. Bendera zilipeperushwa nusu mlingoti katika makao makuu ya Malkia Elizabeth II, Westminister.
Kifo cha Amess kimejiri miaka mitano tangu mbunge mwengine aliyekuwa mwanachama wa chama ya upinzani Labour Jo Cox kuuawa na mtu aliyepandikizwa misimamo mikali ya mrengo wa kulia.
Viongozi watuma risala za rambirambi
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema Amess alikuwa rafiki, mbunge aliyependwa na wengi na mtumishi mwema wa umma.
"Sababu ambayo ninafikiri watu wameshangazwa sana na kuhuzunishwa zaidi ya yote ni kwamba alikuwa mwanasiasa aliyekuwa mnyenyekevu zaidi na mwema sana.”
Jeff Woolnough ambaye ni mhubiri aliyeongoza missa kwa ajili ya marehemu amesema, Amess aliuawa akifanya kile alichopenda kukifanya, kukutana na kushauriana na wapiga kura wa jimbo lake.
Mawaziri wa zamani wa Uingereza walio hai pia walituma rambirambi zao kumuomboleza Amess. "Ni siku ya kutisha kwa demokrasia yetu," amesemaTheresa May.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema kupitia ukurasa wa twitter kwamba shambulizi dhidi ya afisa aliyechaguliwa ni shambulizi dhidi ya demokrasia.
Mjadala kuhusu usalama wa wabunge waibuka tena Uingereza
Amess aliyechaguliwa kwanza wakati wa utawala wa Margaret Thatcher pia alifahamika kutokana na utetezi wake wa haki za wanyama pamoja na masuala ya afya.
Japo mashambulizi ya uma dhidi ya wabunge wa Uingereza si kawaida, katika miaka ya nyuma baadhi wameshambuliwa.
Soma pia: Aliyemuua mbunge Uingereza anatibiwa maradhi ya akili
Mnamo Januari 2000, mbunge wa kiliberali Nigel Jones alijeruhiwa lakini msaidizi wake aliuawa wakati mtu aliyekuwa na upanga kuwashambulia.
Mbunge mwengine Cox aliyeunga mkono Umoja wa Ulaya aliuawa kuelekea kura ya maoni kuhusu Brexit.
Naye Stephen Timms, mbunge wa chama cha Labour alidungwa kisu mara kadhaa mwaka 2010 lakini alipona na angali anahudumu kama mbunge hadi sasa.
(AFPE)