Mauaji ya Mwanaharakati yashindwa kuleta haki Burundi
24 Mei 2012Katika taarifa ya pamoja, mashirika hayo yameilezea hukumu hii kama nafasi iliyopotezwa katika utoaji wa haki na pigo kwa wanaharakati waliokuwa wanaenbdesha kampeni ya kuwawajibisha waliohusika na mauaji ya mwanaharakati huyo wa haki za binadamu.
Ernest Manirumva alikuwa akichunguza kesi kadhaa zinazogusa wakubwa ndani ya serikali ya Burundi wakati alipouawa kinyama mwaka 2009 zikiwemo zinazohusu madai ya rushwa iliyokithiri ndani ya jeshi la Polisi na manunuzi haramu wa silaha.
Mwanaharakati huyo ambaye alikuwa makamu wa rais wa shirika la kuzuia rushwa na na hujumu uchumi (OLUCOME), na pia makamu wa rais wa Taasisi ya kudhibiti manunuzi ya umma alikutwa amekufa nje ya nyumba yake katika Mji mkuu Bujumbura Aprili 9, 2009 baada ya kuchomwa na vitu vyenye ncha kali.
Njia panda
Tangu wakati huo, mamlaka nchini Burundi zimeiacha familia ya mwanaharakati huyo na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa ujumla wakijiuliza kama ukweli wa mauaji hayo utakuja kujulikana siku moja. Lakini Mkrugenzi wa Programu ya Afrika katika shirika la Amnesty International amesema hukumu ya kesi imeshindwa kuweka bayana ukweli huo.
Serikali ya Burundi ilianzisha tume tatu kuchunuguza mauaji hayo na ikakubali msaada kutoka shirika la upelelezi la Marekani FBI kufanikisha upelelezi huo. Tume mbili za kwanza zilikosolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kukosa uhuru na utendaji. Tume ya tatu ilikuwa na ufanisi na kusababisha kukamatwa kwa watu kadhaa. Ripoti ya FBI iliishauri serikali ya Burundi ifanye uchunguzi zaidi ikiwa ni pamoja na kuchukua vinasaba kutoka kwa watu waliotajwa katika ripoti ya FBI.
Lakini Pacifique Nininahazwe ambaye ni mjumbe wa jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali anasema mahakama nchini humo zilikuwa zinapuuza ushauri wa FBI katika kila hatua ya kesi hii na kwamba hakuna hata afisa moja wa Polisi au jeshi aliyetajwa na ripoti ya FBI aliyechunguzwa.
Mbinu chafu
Mawakili wa familia ya marehemu waliomba uchunguzi uhusishe pia mawasiliano ya simu, na kufanya vipimo vya DNA vya watu waliyotajwa kuhusika katika mauaji hayo lakini baada ya kuanza kusikilizwa tena kwa kesi hiyo miezi tisa baadae, Machi 30 mwaka huu, mahakama ilikataa maombi hayo kwa madai kuwa ilitaka isikilize kesi hiyo haraka iwezekanvyo.
Katika kuonyesha ukosefu wa imani na mchakato mzima wa kesi hiyo upande wa mashtaka ulisema utadai fidia kwa sababu mahakama ilikataa vielelezo muhimu. Lakini Gabriel Rufyiri ambaye ni msemaji wa shirika la kupambana na rushwa na hujumu uchumi amesema hawatafanya hivyo.
Katibu Mkuu wa Shirika la kimataifa linalopinga ukandamizaji OMCT Gerald Staberock ameitaka serikali ya Burundi kuonyesha dhamira yake katika kulinda haki za binadamu na watetezi wake kwa kuitendea haki familia ya Ernest Manirumva na shirika lake la OLUCOME.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\HRW Press
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.