Mauaji ya mwanasiasa wa Ujerumani yaibua mjadala
18 Juni 2019Ni kwenye mji huo ambako kundi la manazi la NSU lilifanya mauaji. Na tangu kuuliwa mwanasiasa huyo aliyekuwa mwanachama wa chama cha Christian Social Union (CSU), taarifa nyingi zinazopatikana zinaashiria kwamba aliuliwa kwa sababu za kisiasa. Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali inatuhumu kwamba makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia yamehusika na mauaji hayo.
Mashirika kadhaa ya habari na mitandao ya kijamii imetoa taarifa juu ya mtuhumiwa wa mauaji zinazodai kuwa mtu huyo alikuwa na mahusiano na makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia. Kwa mujibu wa taarifa muhumiwa huyo, mwenye umri wa miaka 45 ana historia ndefu ya uhalifu.
Mtu huyo aliwahi kutoa vitisho dhidi ya serikali. Mwaka uliopita aliandika kwenye mtandao wa Youtube kuitishia serikali kwa kusema ilipaswa kujiondoa madarakani la sivyo yatatokea mauaji.
Vyombo kadhaa vya habari nchini Ujeruamni vimenukulu taarifa zinazobainisha kwamba mtuhumiwa, anayejulikana kama Stephen E alikuwa mwanachama wa makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia ikiwa pamoja na lile la kifashishti mamboleo la chama cha NDP.
Kwa mujibu wa taarifa mtuhumiwa pia alikuwa na mahusiano na kundi linaloitwa Autonomous Nationalists linaloendesha operesheni barani Ulaya kote. Mtu huyo pia aliwahi kuyashambulia maakazi ya wakimbizi kwa bomu mnamo mwaka 1995.
Kutokana na mkasa huo alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela. Pia imeripotiwa kwamba alishiriki katika kuwashambulia watu walioshiriki kwenye maandamano yaliyoandaliwa na jumuiya ya wafanyakazi mnamo mwaka 2009. Kutokana na taarifa hizo,Stephan E. anazingatiwa kuwa mtuhumiwa wa mauaji ya mwanasiasa Walter Lübcke yaliyofanyika tarehe 2 ya mwezi huu.
Kutokana na uchunguzi wa mauji hayo kufanywa na idara ya mwendesha mashtaka mkuu, serikali ya Ujerumani inaupa uzito mkubwa mkasa huo. Kwa kawaida mikasa ya ugaidi huchunguzwa na mwendesha mashtaka mkuu wa serikali.
Msemaji wa vyombo vya habari Markus Schmidt aliwaambia waandishi habari hapo jana kuwa waendesha mashtaka wanayazingtia mauaji ya mwanasiasa Lübcke kuwa yanahusiana na uhalifu wa makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia. Hata hivyo msemaji huo ameeleza kuwa uchunguzi unaendelea.
Mwandishi: Zainab Aziz/Ralf Bosen