1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya Osama yaanza kumkwama Obama

5 Mei 2011

Utawala wa Rais Barack Obama unahangaika kufuta ukungu wa shaka kufuatia taarifa zake juu ya mauaji ya kiongozi wa Al-Qaida yaliyofanywa na wanajeshi wa Marekani mwanzoni mwa wiki hii huko Abbottabad, nchini Pakistan.

Rais Barack Obama wa Marekani
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: dapd

Sasa kile kilichoanza kuonekana kama kisaidizi cha kujenga upya taswira ya Rais Obama kwenye siasa za ndani kimeanza kuchukuwa sura ya kikwazo kutokana na mgongano, na baadhi ya wakati mkinzano, wa taarifa za kifo cha Bin Laden.

Ikulu ya Marekani inasema kwamba kilichosababisha taarifa za mwanzo kuhusiana na kifo hicho zisiwe kamili, ni kile inachokiita "ukungu wa vita".

Kikiwanukuu maafisa wa Ikulu hiyo, kituo cha televisheni cha NBC kimesema kwamba watu wote wanne waliouawa, akiwemo Bin Laden mwenyewe, hawakuwa na silaha.

Taarifa hii ni tafauti kabisa na mbili za mwanzo, ambazo nazo pia zinatafautiana. Ya kwanza ilikuwa ya Rais Obama mwenyewe akitangaza kifo cha Bina Laden, ambayo ilitaja kuwa kiongozi huyo wa Al-Qaida alikufa kutokana na majibizano ya risasi kati yake na makomando wa Marekani. Ya pili kutoka kwa msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jan Carney, ambayo ilisema kuwa si Bin Laden aliyekuwa amejihami kwa silaha, bali ni wenzake wengine.

Wafuasi wa kundi la Jamaat-ud-Dawa la Pakistan wakimsalia Bin Laden sala ya jenezaPicha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo, picha zilizopatikana na Shirika la Habari la Reuters zinaonesha maiti za wanaume watatu zikiwa kwenye madimbwi ya damu, lakini hakuna silaha inayoonekana karibu yao.

Licha ya hayo, Rais Obama amekataa katakata kuchapisha picha za mkasa mzima ulivyokwenda, akirejelea msimamo wa Ikulu yake kwamba huko kutakuwa ni kuchochea zaidi wafuasi wa Bin Laden.

"Hakuna shaka kuwa tumemuua Osama bin Laden. Lakini ni muhimu kwetu kuhakikisha kuwa picha zinazoonesha mtu aliyepigwa risasi kichwani, hazisambai na kuwa kichocheo cha vurugu na silaha ya kufanyia propaganda." Rais Obama alisema hapo jana.

Mwanasheria Mkuu Marekani, Eric Holder, amesisitiza msimamo wa serikali yake kwamba kuuawa kwa Bin Laden hakukukiuka sheria yoyote ya kimataifa, kwani makomando wa Kimarekani walishambuliwa kwanza na ndipo nao wakalazimika kujihami.

Hapo mwanzoni, mauaji haya ya Bin Laden yalianza kuijenga upya taswira ya Rais Obama kwa Wamarekani, ambao waliyapokea kwa vifijo na nderemo wakiamini kuwa kiongozi wao amesimamia kauli yake aliyoitoa tangu mwanzo.

"Nina furaha kwamba tuna rais ambaye amehakikisha kuwa jambo hili kalikamilisha. Na sio rais ambaye amepoteza lengo, kama alivyokuwa George Bush, ambaye badala ya kumshugulikia Osama, akajielekeza Iraq. Nafikiri hivi alivyofanya Obama ndivyo serikali makini inavyotakiwa iwe." Anasema Tyler, kijana wa miaka 30 anayeishi mjini Washington.

Osama bin Laden enzi za uhai wakePicha: AP

Matokeo ya kura ya maoni iliyoendeshwa kwa ushirikiano wa Reuters na kampuni ya Ipsos na kuchapishwa hapo Jumanne, yalionesha kuwa mauaji ya Bin Laden yamepandisha imani ya Wamarekani kwa Rais Obama, ambaye anakabiliwa na uchaguzi hapo mwakani, wakiamini kuwa ameonesha uongozi mzuri panapohusika suala la vita dhidi ya ugaidi.

Lakini kuanza kuibuka kwa taarifa mpya kila siku kuhusiana na namna mauaji yenyewe yalivyotokezea, huku kila taarifa mpya ikipingana na kongwe, kumeanza kuyabadilisha maoni ya watu, si ndani ya Marekani tu, bali hata nje.

Nchini Pakistan, ambako ndiko Osama alikouawa, kumekuwa na maandamano makubwa. Chama kikuu cha upinzani nchini humo, Jamaat-e-Islam, kimeitaka serikali ya Pakistan ijitowe kwenye ushirika na Marekani kupambana na ugaidi na kimeitisha maandamano makubwa hapo kesho, baada ya sala ya Ijumaa.

Mwandishi: Rüdiger Paulert/WDR/Reuters
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi

Gundua zaidi

Onesha taarifa zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW