1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya raia 71 yazua hofu na hasira Ntoyo, DRC

12 Septemba 2025

Mauaji ya watu 71 yaliyofanywa na waasi wa ADF siku ya Jumatatu katika kijiji cha Ntoyo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, yamezua hisia kali za hofu, hasira na majonzi miongoni mwa wakaazi.

Demokratische Republik Kongo Beni 2024 | Gemeinsame Operation ugandischer und kongolesischer Truppen
Wanajeshi wa Uganda (UPDF) na wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) katika operesheni ya pamoja dhidi ya waasiPicha: Philemon Barbier/AFP/Getty Images

Mauaji ya raia 71 yaliyofanywa na kundi la waasi wa ADF Jumatatu wiki hii mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yameibua hisia mseto za hofu na hasira miongoni mwa wakaazi wa kijiji cha Ntoyo.

Wanasema madai ya jeshi la nchi yao na yale ya Uganda kwamba wamewatokomeza waasi hao si kweli kwa sababu waasi hao wanaendelea kuwaua watu na kuharibu mali zao.

Siku ya Jumatatu, wakaazi wa kijiji cha Ntoyo chenye idadi ya watu 2,500 hivi walivamiwa na waasi wa ADF walipokuwa wakijiandaa kushiriki mazishi.

Kulingana na walionusurika mauaji hayo watu hao 71 walichinjwa na wengine waliuawa kwa kuchomwa moto. Wakaazi hao wameyataja mauaji hayo kuwa ya kikatili zaidi hivi karibuni yakifanywa na kundi hilo la waasi wa ADF.

Kijiji cha Ntoyo kilichokuwa na wakaazi 2,500, sasa kimebaki kitupu

Kufikia katikati ya wiki, kijiji cha Ntoyo kilikuwa hakina watu kwani idadi kubwa waliyakimbia makazi yao kwa hofu ya mashambulio zaidi.

Wakaazi wengi walikimbia kwa hofu ya kutokea mashambulizi zaidi, wakijificha misituni au kukimbilia miji ya jirani kama Manguredjipa, ulioko kilomita 7 kutoka kijiji cha Ntoyo.

Samuel Katsuva Mumbere ni mkaazi wa Ntoyo, "Tunakimbia kuongezeka kwa mashambulizi. ADF walituvamia na unaona watu wengi waliuawa, hali ambayo inatutia hofu na wasiwasi na kutulazimisha kuyakimbia makazi yetu."

Takriban wakimbizi 7,000 wa Kongo wamevuka mpaka na kuingia Uganda kufuatia mashambulizi ya waasi wa ADF mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Nicholas Kajoba/Xinhua/IMAGO

Takriban maiti za watu kumi zilibaki katika sehemu kulikotokea mauaji hayo huku jamaa wakiendelea kuwatafuta watu wao kuweza kuwafanyia maziko.

Wakaazi wamelikosoa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kushindwa kuwadhibiti ADF. Wanalilaumu pia jeshi la Uganda ambalo mara kadhaa limedai kuwatokomeza waasi hao.

Kati ya tarehe 13 na 14 mwezi huu, waasi wa ADF waliwaua raia wengine zaidi ya 40 walipovamia miji kadhaa eneo la Manguredjipa. Hata hivyo msemaji wa jeshi la Kongo Luteni Marc Elongo eneo la Kivu Kaskazini ameelezea kuwa mbinu mpya wanazotumia ADF zinawasababishia changamoto ya kuwakabili.

Je,Uganda inachochea mzozo wa mashariki ya Kongo?

01:56

This browser does not support the video element.

"Adui wanaandamwa katika pori na kwa hakika tunawapa shikinizo. Ili kukwepa shinikizo kutoka kwa majeshi yetu pamoja na jesho la Uganda, wameamua kujigawanya katika vikundi vidogo na kuvamia kutoka kule tunakotoka. Kwa kufanya hivyo inamaanisha wako dhaifu na hawawezi kukabiliana nasi moja kwa moja."

Kwingineko katika jimbo la Kasindi idadi ya watu walioambukizwa ugonjwa wa Ebola imeongezeka kutoka watu 28 hadi 68 katika kipindi cha wiki moja tu tangu mlipuko wa ugonjwa huo ulipothibitishwa.

Ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo, mamlaka zimewazuia watu kusafiri katika maeneo ambayo yamo hatarini hasa yale yaliyo jirani na mji mkuu wa jimbo la Kasai, Tshikapa.

Shirika la Afya duniani WHO limesema limewapeleka wataalamu katika jimbo la Kasai ili kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa, kutoa matibabu na kufuatilia hatua za kuzuia na kudhibiti wa maambukizi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW