1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya Solingen na ustawi wa kina mama wadogo Ujerumani

7 Septemba 2020

Mauaji ya watoto watano yanayodaiwa kufanywa na mama yao mjini Solingen, Ujerumani yanazusha maswali mengi. Ni vipi mauaji hayo yangeweza kuzuiwa? Na kwa nini msaada kwa akina mama vijana Ujerumani unaonekana hautoshi?

Deutschland Solingen | Trauer um den Tod von fünf Kindern
Picha: Imago Images/O. Krschak

Uchunguzi wa mauaji hayo ya Solingen ndiyo kwanza umeanza. Mama huyo anaaminika aliuwaua watoto wake watano kati ya sita alionao kabla ya yeye mwenyewe kujaribu kujiuwa. Watoto hao wana umri wa miaka minane, sita, mitatu, miwili na mmoja.

Maelezo ya kesi hii bado hayajakamilika. Haifahamiki sana mazingira ambayo familia hii iliishi. Hakuna kinachojulikana kuhusu lengo la mauaji hayo, achilia mbali njia ambazo zingetumika kulizuia janga hilo.

Lakini ukweli kwamba mwanamke huyo alimpata mtoto wake wa kwanza mwenye umri wa miaka 11 akiwa na umri wa kati wa ujana, ghafla umeweka mkazo kuhusu msaada unaotolewa kwa ajili ya akina mama wadogo nchini Ujerumani.

Ushauri nasaha bila malipo na unaweza kuwa siri

Akina mama vijana wana haki kisheria ya kupata ushauri nasaha nchini Ujerumani. Huduma za ustawi wa vijana za majimbo, mashirika yasiyo ya kiserikali na makanisa, yanatoa msaada na ushauri bila malipo.

Washauri wanawasaidia vijana ambao ni wajawazito kuomba msaada wa kifedha, kuwatafutia nyumba, kuwatatulia matatizo na waajiri wao au shule na kuwapatia huduma za watoto.

Mshauri katika ofisi ya ustawi wa vijana atatathmini mazingira ya kuishi ya vijana wajawazito: Bado anaenda shule au anamalizia mafunzo ya ufundi stadi? Kama anaishi na wazazi wake, anaweza kuishi hapo na mtoto wake na kupata msaada? Anahitaji msaada wa kifedha? Na kiasi gani baba atahusika katika malezi na kutoa msaada wa kifedha kwa mtoto?

Kwa mfano mjini Solingen, Idara inayohusika na nyumba kwa Mama na Mtoto inatoa makaazi ya muda kwa hadi akina mama wanane wenye watoto wenye umri wa miaka sita au chini ya hapo.

Polisi wakiizingira nyumba ambako miili ya watoto watano iligundulikaPicha: picture-alliance/AA/M. Zeyrek

Ofisi ya ustawi wa vijana pia inakusudia kusaidia katika utunzaji wa mtoto. Lengo likiwa siku zote kuziwezesha familia ndogo kujitegemea. Kama wazazi wote wana umri chini ya miaka 18, ofisi ya ustawi wa vijana inachukua rasmi malezi ya mtoto, inashughulikia taratibu zote kisheria na masuala ya kifedha hadi mama atakapofikisha miaka 18.

Je msaada hauwafikii walengwa?

Mashirika kadhaa yameanzishwa kuhakikisha watoto wanapata maisha mazuri. Shirika la Msaada wa Awali, lililoanzishwa na Wizara ya Vijana na Masuala ya Familia ya Ujerumani mwaka 2007 linalenga kuimarisha hali za watoto walio chini ya miaka mitatu. Pia linatoa msaada wa mafunzo kwa washauri nasaha na wafanyakazi wa ofisi ya ustawi.

Msemaji wa shirika la misaada la Kanisa Katoliki Caritas nchini Ujerumani, Mathilde Langendorf ameiambia DW kwamba mjini Solingen wanazihudumia familia kadhaa, ambapo wafanyakazi wa huduma za watoto huzitembelea familia na kutoa ushauri kwa akina mama wanaolea watoto peke yao.

Kuongezeka kwa unyanyasaji na kushindwa kutunza

Mjini Solingen majirani waliiambia DW kuhusu mabishano na vurugu kati ya mama na mpenzi wake. Lakini bado haijafahamika kama mauaji hayo yanahusiana na kushindwa kuwatunza watoto au unyanyasaji.

Shirika la kuwalinda watoto nchini Ujerumani limeonya dhidi ya uchunguzi wa mapema wa kisa cha sasa. Msemaji wa shirika hilo, Juliane Wlodarczak ameiambia DW kwamba asili ya mauaji haya haijulikani, hawajui aina ya msaada iliyokuwa inapata familia hiyo, kama ofisi ya ustawi ilikuwa tayari inahusika au kama mama alijaribu kupata msaada wowote.

Shirika hilo la kuwalinda watoto linaamini kwamba katika hali kama hiyo watu wanapaswa kutulia na kuchukua muda kuwaomboleza wahanga na kujizuia kurukia katika hitimisho.

(DW)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW