1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji yatikisa jamii za Kaskazini mwa Uganda

5 Aprili 2022

Jamii zilizoko kanda ya Kaskazini Mashariki mwa Uganda zinaishi katika hofu kubwa kufuatia wimbi la mauaji ya watu pamoja na wizi wa mifugo kwenye eneo hilo. Wanaotenda uhalifu huo wanatajwa  kuwa jamii ya Karamojong.

Uganda Kaabong Wahlen Karamojong Volk
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Wanaotenda uhalifu huo wanatajwa  kuwa watu wa  jamii ya wafugaji wa kuhamahama wa Karamojong, ingawa  jamii hiyo inakanusha tuhuma hizo ikidai mauaji ya raia na wizi wa mifugo vinafanywa na jeshi la Uganda pamoja na jamii kutoka nchi jirani ya Kenya.

Mfugaji wa jamii ya Karamojong nchini Uganda Picha: DW/F. Yiga

Mwandishi wa habari wa shirika la URN Edward Eninu amenusurika katika jaribio la uvamizi wa mchana uliofanywa na wezi wa mifugo wilaya ya Kapelabiong. Alikuwa akifuatilia taarifa za wezi hao kuvamia soko la mifugo eneo hilo lakini akajikuta katika hatari na kukimbilia usalama wake.

Tangu mwezi Machi, jamii ya Karamojong na zile za Teso, Lango na Acholi zinazopakana nayo zimekumbwa wa wimbi jipya la wizi wa mifugo na mauaji ya watu ambayo yanadaiwa kufanywa na wezi wa mifugo. Jeshi la Uganda limethibitisha kuua idadi kubwa ya wezi wa mifugo wakidaiwa kutokea nchi jirani ya Kenya na kushirikiana na wenzao wa Karamoja.

Tamasha la utamaduni wa Wakaramoja

02:37

This browser does not support the video element.

Msemaji wa jeshi la Uganda Kanali Felix Kulayigye amethibitisha idadi ya waliouawa katika operesheni ijulikanayo "Usalama kwa wote" inayoenda sambamba na kuwapokonya raia silaha haramu.

Mwandishi habari Edward Eninu amesema kuwa mauaji ya raia yanafanyika hata nje ya kanda ya Karamoja katika visa vya uvamizi unaolenga kupora mifugo.

Ila wanasiasa kutoka kanda ya Karamoja wanawalaumu majeshi kwa kuwaua hata raia wasio kuwa na hatia baada ya kuwatesa kikatili. Wanaelezea kuwa kanda ya video ambayo imesambazwa na askari wakisherehekea ushindi wakitumia sehemu za miili ya watu ni kielelezo tosha kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika operesheni ya kukabiliana na wezi wa mifugo.

Lakini msemaji wa majeshi kanda ya Kaskazini Mashariki Meja Issac Owere amekanusha madai hayo akiwataka wanasiasa washirikiane na majeshi kukomesha uhalifu eneo hilo.

Msemaji wa majeshi Kanali Felix Kulayigye amefichua kuwa tangu walipoanza operesheni ya kutwaa silaha haramu mwezi Julai mwaka uliyopita, bunduki 192, risasi zaidi ya 23,000 pamoja na mifugo zaidi  ya 16,000 vimekombolewa kutoka kwa wezi wa mifugo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW