Mauwaji ya mwaka 1972 yakumbukwa Olimpiki
7 Agosti 2012Uingereza ambayo ni mwenyeji wa michezo hiyo hadi sasa imeshajikusanyia medali 18 za dhahabu. Katika riadha, James Grenada alishinda fainali ya mbio za mita 400 wanaume. Mambo hayakuwa mazuri kwa Ujerumani baada ya Silke Spiegelburg na Martina Struzt kushindwa kupata ushindi kwenye mchezo wa kuruka na upondo na hatimaye wakaambulia nafasi za nne na tano.
Mzimu wa kupoteza uliiandama tena Ujerumani katika mchezo wa mpira wa mezani, baada ya kikosi cha China kufanikiwa kufika fainali na kuiacha Ujerumani iwanie medali ya shaba kesho Jumatano.
Jana kulifanyika pia tukio la kumbukumbu ya mauwaji ya wanamichezo wa Israel miaka 40 iliyopita katika michezo ya mjini Munich hapo mwaka 1972.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle na mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, IOC, Jacques Rogge, walishiriki katika tukio hilo.
Septemba 5, mwaka 1972 kundi la wanamgambo wa Kipalestina liliwakamata mateka wanamichezo wa Israel, ambapo kumi na moja kati yao waliuwawa pale jaribio la kuwaokoa liliposhindwa.
Suala ya kuwakumbuka wanamichezo hao lilizua mjadala kabla ya kuanza kwa michezo ya Olimpiki ya mwaka huu baada ya wanafamilia wa waliouawa kutaka kukumbukwa kwa wapendwa wao huku baadhi ya wadau wakidai kufanya hivyo ni kuchanganya michezo na siasa.
Japan yajizatiti kulinda heshima yake
Katika upande wa soka, Japan na Marekani zimefanikiwa kutinga nusu fainali ya soka la wanawake kwenye mashindano hayo. Japan iliishinda Ufaransa kwa bao 2-1 huku Marekani ikiichapa Canada 4-3 kwenye mchezo uliokwenda hadi muda wa ziada katika uwanja wa Old Trafford jijini Manchester.
Japan itajikakamua vilivyo kwenye mchezo wa nusu fainali ili kuuthibitishia ulimwengu kuwa ushindi wake wa Kombe la dunia kwa wanawake mwaka uliopita haukuwa wa kubahatisha.
Felix Sanchez kutoka Jamhuri ya Dominican alifanikiwa kutwaa medali ya dhahabu kwenye mbio za kuruka viunzi mita 400 kwa wanaume baada ya kumzidi uwezo Mmarekani Michael Tinsley. Hii ni mara ya pili kwa Sanchez mwenye umri wa miaka 34 kutwaa medali hiyo ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni miaka nane iliyopita.
Masumbwi nayo yamekuwa na hamasa kubwa kwenye michezo ya mwaka huu hasa kwa upande wa wanawake ikizingatiwa kuwa ni mara ya kwanza kuingizwa kwenye orodha ya michezo hiyo.
Mwanamama askari kutoka India Mary Kom alifanikiwa kutwaa ushindi kwenye mchezo huo baada ya kumtwanga makonde ya nguvu mshindani wake Maruua Rahali wa Tunisia. Kom aliwaambia waandishi wa habari kuwa ameukaribisha kwa heshima uamuzi wa kamati ya olimpiki kuujumuisha mchezo huo.
Yanayojiri leo
Hii leo duru ya kwanza ya mbio za wanawake mita 5000 itaanza pamoja na nyingine za mita 200 wanaume na wanawake, 100 kuruka viunzi wanawake, nusu fainali ya mita 800 kwa wanaume.
Marekani inakibarua cha kulinda heshima yake kwenye mchezo wa mpira wa kikapu katika robo fainali ya timu za wanawake dhidi ya Canada. Michezo mingine ni pamoja na mpira wa wavu, ngumi pamoja na kuogelea.
Mwandishi: Stumai George/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef