1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauwaji ya Waasi kaskazini ya Mali

14 Februari 2012

Jumuia ya kimataifa imelaani vikali mauwaji ya kinyama yaliyofanywa na waasi wa Touareg kaskazini mwa jamhuri ya Mali.Mapigano katika eneo hilo yamepelekea maelfu ya watu kuyapa kisogo maskani yao.

Manöver des malischen Militärs gegen den islamistischen Terrorismus im Sahel; die malische Armee wird dabei von westlichen Militärexperten beraten
Luteka za jeshi la MaliPicha: picture-alliance/Désirée von Trotha

Wanajeshi kadhaa wa serikali na raia wa kawaida wameuliwa huko Aguelhok,kaskazini mashariki ya jamahuri ya Mali tangu waasi wa Touareg walipoanza hujuma zao kati kati ya mwezi uliopita.

Ripoti ya waziri wa ushirikiano wa Ufaransa,Henri de Raincourt kuhusu mauwaji hayo,imethibitishwa na jeshi la Mali mjini Bamako.

"Mauwaji ya kinyama yamefanyika huko Aguelhok,wanajeshi,raia wa kawaida,inasemekana watu wasiopungua mia moja,walitekwa nyara na baadae kuuliwa kikatili kabisa" amesema waziri waziri huyo wa ushirikiano wa Ufaransa.

Henri der Raincourt aliyeitembelea Mali february tisa iliyopita hakutaja nani walikuwa nyuma ya mashambulio hayo,alisema tu mtindo wa mauwaji hayo unalingana na ule unaotumiwa na Al Qaida."

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa,Alain Juppé, nae pia amelaani mauwaji hayo akisema lakini"haijulikani bado nafasi iliyoshikiliwa na Al Qaida au Aqmi katika mashambulio hayo.

Wahamiaji wa TouaregPicha: AP

Mkuu wa idara ya upelelezi na uhusiano wa jamii nchini Mali,kanali Idrissa Traoré amethibitisaha mauwaji ya kinyama yaliyofanyika january 24 huko Aquelhok na kuongeza;raia pia wameuliwa.

"Mauwaji ya kikatili yametokea siku hiyo,watu wamekatwa vichwa,wengine wamepigwa risasi kichwani,kulikuwa na hata raia miongoni mwa wahanga wa mauwaji hayo ambayo hayawezi kufanywa na yeyote mwengine isipokuwa wafuasi wa Al Qaida katika eneo la maghreb-Aqmi" amesema mkuu huyo wa idara ya upelelezi ya Mali.

Hakutaja idadi halisi ya wahanga lakini afisa mmoja wa jeshi aliyeshiriki kuwazika wahanga hao amesema wanajeshi 97 wameuliwa.

January 26 iliyopita serikali ya Mali ilisema wafuasi wa Aqmi na waasi wa Touareg washambulia kwa pamoja mji wa Aguelhok.

Aguelhok,mji ulioko kilomita 150 kaskazini mashariki ya Kidal umegeuka kuwa kitovu cha mapigano yaliyopelekea watu wasiopungua elfu nne kuyapa kisogo maskani yao.

Tume ya shirika la kimataifa la Msalaba mwekundu na lile la Mali imefika katika maeneo walikokimbilia wakimbizi hao ili kuwahudumia.

Kasri la rais wa Mali mjini BamakoPicha: picture-alliance/dpa

Kuna maelfu waliotawanyika ndani nchini Mali na wengine waliokimbilia Mauritania,Niger na Burkina Faso.

Jana rais Amadou TOumani Toure wa Mali alifanya ziara fupi mjini Ouagadougou na kuzungumza na kiongozi mwenzake wa Burkina Faso Blaise Compaore ambae nchi yake inawapokea wakimbizi elfu kumi wa Mali.Miongoni mwa wakimbizi hao kuna wanajeshi akiwemo mkuu wa vikosi vya gendarmerie aliyetangaza hivi karibuni kudai uhuru wa eneo la kaskazini la Mali.Serikali ya Mali inataka mwanajeshi huyo anyamazishwe au arejeshwe nyumbani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW