1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauzo ya nje ya silaha ya Ujerumani yaongezeka

Sekione Kitojo
24 Januari 2018

Kwa mujibu wa ripoti mpya, serikali ya Ujerumani imeidhinisha mauzo mengi ya silaha kwenda katika nchi za mizozo. Serikali ya vyama vya CDU na SPD pia iliweka rekodi mpya ya mauzo ya silaha, licha ya ahadi za kupunguza.

Infografik Waffenexporte 2012 - 16 Englisch

Serikali  hiyo  ya  muungano  imeidhinisha  mauzo mengi ya  silaha  katika  muda  wa  miaka  minne, na  kuzusha  mjadala  juu ya  sera  ya  nchi  hiyo  ya  mauzo  ya  silaha.

Serikali  ya  kansela  Angela  Merkel  imeidhinisha  zaidi  ya  mauzo ya  silaha  yenye  thamani  ya euro bilioni 25.1  sawa  na   dola  za Kimarekani  bilioni 30.9 tangu  kuingia  madarakani  mwaka  2014.

Vifaru vilivyoundwa nchini Ujerumani Picha: picture-alliance/dpa/B. Settnik

Hii  inaifanya  serikali  ya  sasa , muungano  kati  ya  chama  cha kansela  Merkel  cha  Christian Democratic, CDU  na  kile  cha siasa  za  wastani  za  mrengo  wa  kushoto cha  SPD , kuwa imefanya  mauzo  zaidi kuliko  serikali  yoyote  ya  Ujerumani   katika enzi  za  sasa, kituo  cha  televisheni  cha  taifa  ARD  kimeripoti.

Mabadiliko  muhimu  yamekuja  katika  mauzo  kuelekea  katika mataifa  nje  ya  Umoja  wa  Ulaya  na  NATO , serikali  ya  mjini Berlin  iliidhinisha  mauzo  ya  silaha  yenye  thamani  ya  euro bilioni  14.48 kati  ya  mwaka  2014  na  2017. Hii  ni  ongezeko  la asilimia 47 ikilinganishwa  na  baraza  la  mawaziri  la  mwaka  2010-2013.

Kabla  ya  makubaliano  ya   kuundwa  kwa  serikali  ya  mseto mwaka  2013, chama  cha  SPD kiliahidi  kuweka  sheria  kali katika mauzo  ya  silaha. Makubaliano  hayo  pia  yalisababisha  kuwekwa Sigmar Gabriel  wa  SPD   kuwa  mkuu  wa  wizara  ya  uchumi , na kumpa  nafasi  ya  kuangalia  mauzo.

Vifaru vilivyotengenezwa nchini Ujerumani Picha: picture-alliance/dpa/U. Zucchi

Mauzo ya nje ni  makubwa

Kituo cha  televisheni  cha  ARD  cha  Ujerumani  kimesema  ripoti yake  imo  katika  misingi  ya  data  zilizotolewa   na  wizara  ya uchumi, kufuatia  uchunguzi  uliofanywa  na  chama  cha  Die Linke.

Kituo  hicho  cha  televisheni  kimesema  data  hizo ni  za  awali na kwamba  idadi hiyo  inaweza  kuongezeka.

"Miaka  minne  iliyopita, SPD iliahidi  kujiweka  mbali  na  sera  ya mauzo  ya  nje  ambayo yatakuwa  katika  msingi  wa  uchumi," Stefan  Liebich  kutoka  chama  cha  Die Linke alikiambia  kituo cha ARD.

"Katika  hali  ya  kawaida,  milango  haikufungwa , lakini  ilifunguliwa wazi  zaidi."

Vifaru vya UjerumaniPicha: Imago/teutopress

Kiongozi  huyo  wa  wabunge  wa  chama  cha  Die Linke  Dietmar Bartsch alikwenda  umbali  zaidi  leo (jana), kwa  kusema ni  vigumu kuamini  kwamba  Ujerumani  itapeleka  silaha  kwa  mataifa yanayoongozwa  na  madikteta.

"Tarakimu  ambazo  zimechapishwa  hivi  sasa  zinaonesha  kwamba kuna  hatua  pia  kuporomoka  kwa  uadilifu  ambao  sijawahi kufikiria  kuwa  unawezekana," Bartsch  alisema, akielezea  mauzo hayo  kuwa  ni "kushindwa  kwa  jumla" kwa  serikali  ya  muungano.

Mwanasiasa  huyo  wa  siasa  za  mrengo  wa  kushoto  alisema usafirishaji  wa  silaha  kutoka  Ujerumani  kwenda  Uturuki kunahitajika  kusitishwa  mara  moja."

Chama  cha  Kijani  cha  Ujerumani  pia  kimeikosoa  vikali  serikali , kikisema  kushindwa  kwao kuzuwia  mauzo  ya  nje  ya  silaha  ni ishara  ya   kuwa  "muflisi".

Sheria za  mauzo

Baraza  la  mawaziri  limekuwa  likikiuka  sheria  zake  wenyewe katika  mauzo  ya  nje  ya  silaha, alisema  mtaalamu  wa  chama hicho  wa  masuala  ya  sera  za  nje Omid Nouripour, licha  ya mahubiri  aliyotoa  kwa   Sigmar  Gabriel.

Mnunuzi  mkubwa  wa  silaha  za  Ujerumani  ni  Algeria , ambayo imenunua  kiasi  cha  silaha  zenye  thamani  ya  euro bilioni 1.36 katika  miaka  ya  hivi  karibuni.

Ndege za kivita za UjerumaniPicha: picture-alliance/Photo Shot/B. Photo

Orodha  ya  mataifa  kumi  ina  mataifa  matatu  ya  mashariki  ya kati  yanayohusika  katika  mzozo  nchini  Yemen, Misri, Saudi Arabia  na  Umoja  wa  falme  za  Kiarabu.

Ripoti  hiyo  inakuja  wakati  mgumu  wa  matatizo  kwa  serikali  ya Ujerumani , huku  kukiwa  na  kelele  zilizozushwa  na  picha  ya vifaru  vilivyoundwa   Ujerumani  vikipelekwa  nchini  Syria  na majeshi  ya  Uturuki. Hali  hiyo  pia  inaleta  shaka  kuhusu mazungumzo  ya  hivi  karibuni  kati  ya  chama  cha  CDU  na  SPD kuhusu  kuunda  serikali  ijayo  ya  Ujerumani, ambayo  pia inajumuisha  ahadi  ya  kuweka  sheria  kali  kuhusiana  na  mauzo ya  silaha.

Mwandishi: Sekione  Kitojo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW