1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Utawala wa sheriaTanzania

Mawakili wajadili juu ya kulindwa kwa utawala wa sheria

11 Julai 2024

Jumuiya ya Mawakili wa Afrika Mashariki imejadili namna ambavyo wanahabari, wanasheria na asasi za kiraia, zinavyoweza kuhamasisha kulindwa kwa utawala wa sheria, haki za kiraia na sheria zinazosimamia uhuru wa habari.

Symbolbild | Justiz
Nyundo ya mahakamani ni ishara ya hakiPicha: fikmik/YAY Images/IMAGO

Wanasheria hao kutoka Jumuiya ya mawakili wa Afrika Mashariki leo wamekutana na wanahabari na asasi za kiraia mjini Dar es Salaam, ili kuangalia kwa pamoja namna ambavyo nchi wanachama zinavyoweza kuchochea mabadiliko katika sheria zinazominya uhuru wa habari na upatikanaji wa taarifa hasa katika zama za kidijitali.

Katika warsha hiyo, wanasheria hao walichambua sheria mbalimbali za Tanzania ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari, sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi, sheria ya udhibiti wa Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta pamoja na sheria nyingine  kadhaa za mataifa ya Afrika Mashariki.

Soma pia: Wadau wa siasa nchini Tanzania walalamikia sheria za uchaguzi nchini humo

Akizungumza katika warsha hiyo, Meneja Programu na wakili kutoka Uganda, Gabriel Achaye, amesema:

"Leo tuna majadiliano makubwa kuhusu haki za kidijitali, tunataka kujadili, masuala ya utunzaji wa taarifa binafsi, uhuru wa watu kujieleza hasa wanahabari na asasi za kiraia, kwa sababu wanahabari ni sauti kwa wasio na sauti."

Wadau wa Habari na wa teknolojia, nchini Tanzania kwa muda mrefu wamekuwa wakipigia upatu kuwepo mabadiliko ya sheria zinazodaiwa kuminya uhuru wa Habari ikiwamo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu za kupata habari

Waandishi wa habari nchini Kenya wakifuatilia sherehe za siku ya wafanyikazi duniani mjini NairobiPicha: Billy Mutai/SOPA Images/ZUMA Wire/picture alliance

Akizungumza katika warsha hiyo, Mkurugenzi wa programu kutoka EALS, Achilles Romward amesema jumuiya hiyo, inasimamia kuwajengea uelewa wadau kujua haki zao za kikanda, ili waweze kuzipigania na kuzidai.

Mkurugenzi wa Jukwaa la Asasi za kiraia, Tanzania (Nacongo) Rachel Chagonja, amesema, "Kazi yetu sisi ni kuchagiza mijadala inayohusiana na sera na sheria zinazoongoza mitandao ya kijamii na uhuru wa kujieleza."

Katikati ya mjadala kuhusu sera na sheria, zinazominya uhuru wa Habari na upatikanaji wa taarifa, katika zama za kidijitali Mwanahabari nguli wa Tanzania, Jenerali Ulimwengu alikuwa na mtazamo huu.

Soma pia: Mjadala kuhusu sheria ya uchaguzi Tanzania bado wafukuta

"Mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu sana inakupa taarifa nyingi, kwa wakati na kwa kasi, na inakuwezesha kupata habari nyingi katika muda mfupi, lakini hata hivyo inabidi itumike ikiwa na usuli wa utu na maadili na uadilifu."

Jumuiya ya mawakili wa Afrika Mashariki, ilianzishwa 1995, na taasisi za wanasheria kutoka nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki,ikiwa na lengo la kuwaleta pamoja wanasheria ili kushirikishana sheria za Afrika Mashariki, kanuni za masoko Afrika Mashariki, kuimairisha utawala wa sheria na fursa zilizoko katika ukanda huo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW