Mawakili wa Kenyatta waendelea kutoa hoja zao
6 Februari 2014Mawakili wanaomuakilisha Rais Uhuru Kenyatta leo wanatoa hoja zao mbele ya majaji wa mahakama hiyo wanaoongozwa na Jaji Kuniko Ozaki.
Wakili Steven Kay amesema kesi hiyo kwa sasa haina nguvu na kutaka ifutiliwe mbali kutokana na kuahirishwa kwa kesi iliotarajiwa kuanza hapo jana, baada ya Mwendesha Mashataka Mkuu Fatou Bensouda kusema hana ushahidi wa kutosha wa kuendeleza kesi hiyo.
Mawakili wa Rais Kenyatta wanahoji kuwa Bensouda anaendelea kuiburuta kesi hiyo akijua wazi kwamba hata baada ya kupewa muda zaidi, bado hatoweza kukusanya ushahidi dhidi ya mteja wao.
Kenyatta, aliye na umri wa miaka 52 na ambaye ndiye rais wa kwanza anayeshitakiwa katika mahakama hiyo wakati akiwa madarakani, anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binaadamu yanayodaiwa kufanyika katika ghasia za baada ya uchaguzi zilizofanyika mwaka wa 2007/2008, ambapo zaidi ya watu 1,200 waliuwawa.
Bensouda aomba kesi isifutiliwe mbali
Katika mkutano huo wa kusikiliza hoja za pande zote ulioanza jana katika makao makuu ya mahakama hiyo ya ICC mjini Hague, Uholanzi, Mwendesha Mashtaka aliiomba mahakama kutoifutilia mbali kesi hiyo huku akitoa hoja zake na kudai serikali ya Kenya haitoi ushirikiano kamili hatua inayomtatiza katika kukusanya ushahidi wake.
Bensouda amesema kitu anachohitaji kwa sasa ni kupata stakabadhi za benki za Rais Kenyatta ambazo zitatoa ushahidi wa rais huyo kufadhili ghasia hizo za baada ya uchaguzi.
Aidha Bensouda alitaka mahakama hiyo iridhie kuiahirisha kwa mara nyengine tena kesi hiyo kwa miezi mitatu ili kutoa muda kwa upande wake kujitayarisha na kudhibiti ushahidi wa kutosha dhidi ya kesi hiyo.
Huku hoja hizo zikiendelea kusikilizwa baadhi ya waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi, wameanza kuingiwa na wasiwasi juu ya kupatikana kwa haki, ikiwa mahakama itaaamua kuifutilia mbali kesi hiyo.
Wakili anayewawakilisha waathiriwa hao, Fergal Gaynor, ameishutumu serikali ya Kenya kwa kujaribu kusambaratisha kesi hiyo.
Kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto pamoja na mwanahabari JoShua Arap Sang imeendelea kukumbWa na matatizo kadhaa yakiwemo ya kuahirishwa.
Hii inajumuisha pia madaia ya kutishwa kwa mashahidi na kujiondoa katika kesi hiyo na hata baadhi ya mashahidi kudaiwa kutoa ushahidi wa uongo, huku serikali ya Kenya ikiendelea kufanya kampeni ya kimataifa ya kutaka kuisimamisha kesi hiyo.
Kwa sasa hatma dhidi ya kesi ya Uhuru Kenyatta itategemea na namna majaji katika kesi hiyo watakavyoshawishika aidha kuitupilia mbali au kuiahirisha kwa miezi mitatu.
Mwandishi: Amina Abubakar/The Daily Nation/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef