Mawaziri AU wapendekeza fidia ya mabilioni ya dola kwa Afrika
25 Agosti 2009Katika kikao hicho mawaziri hao wametoa pendekezo kwa wakuu wa nchi za kiafrika, kudai fidia ya kiasi cha dolla billioni 67 kwa mwaka kutoka kwa mataifa yaliyoendelea, kutokana na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa ambayo bara hilo limeyapata.
Rasimu ya azimio hilo, lililoandaliwa na mawaziri hao, linataka fidia ifikie kiwango hicho cha dolla billioni 67 kianze kulipwa mwaka 2020.
Akizungumza katika kikao hicho,Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Jean Ping amesema ni wakati muafaka sasa kwa Afrika kushiriki kikamilifu kuhakikisha kuwa suala la mabadiliko ya hali ya hewa linapewa umuhimu mkubwa.
Maafisa wa Umoja wa Afrika wanasema kuwa katika siku za nyuma kumekuwa na ugumu katika uwezo wa Afrika katika majadiliano ya mabadiliko ya hali ya hewa kutokana na serikali za kiafrika kutokuwa na msimamo wa pamoja.
Rasimu ya mapendekezo ya mawaziri hao inasema kuwa kunahitajika uungwaji mkono wa wanasiasa kwa watalaam wanaoshiriki katika majadiliano, kuhakikisha kuwa sauti ya Afrika inasikika vilivyo na kutiliwa maanani.
Mabadiliko ya hali ya hewa yameiathiri sana Afrika
Ikumbukwe ya kwamba Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, limeonya kuwa ifikapo mwaka huo wa 2020, takriban watu millioni 250 barani Afrika watakabiliwa na uhaba wa maji.
Tafiti zimeonesha kuwa Afrika inabeba mzigo mkubwa wa madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa, pamoja na ukweli , kuwa bara hilo limechangia kiasi kidogo cha utoaji wa gesi inayoharibu mazingira.
Bara hilo linatarajiwa kuathiriwa vikali na kuongezeka kwa kiwango cha bahari, ukame, pamoja na mafuriko, iwapo ongezeko la ujoto duniani halitadhibitiwa.
Tayari wanaharakati wametanabaisha kuwa ukame wa muda mrefu unatishia mamillioni ya watu katika pembe ya Afrika katika baa la njaa, hali ambayo inadhihirisha madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Mapendekezo
Mapendekezo yaliyotolewa na wanaharakati wa mazingira yanayataka mataifa yaliyoendelea kupunguza utoaji wa gesi inayoharibu mazingira kwa asilimia 40, kutoka katika kiwango kilichowekwa mwaka 1990 ndani ya kipindi cha miaka kumi ijayo.
Mkutano wa mwezi Decemba huko Copenhagen ni sehemu ya mpango unaelenga katika majadiliano ya kufikiwa kwa mkataba mpya wa kupambana na mabadiliko ya hali, mkataba ambao utachukua nafasi ya ule wa sasa wa Kyoto ambao unamalizika mwaka 2012.
Mataifa ya Afrika yamekuwa yakijaribu kufikia msimamo wa pamoja na azimio katika kuongeza mbinyo wa kutimizwa kwa matakwa ya bara hilo.
Rasimu ya azimio hilo iliyotayarishwa na mawaziri hao, inatarajiwa kujadiliwa pembezoni mwa kikao maalum cha Umoja wa Afrika cha Amani na Usalama kitakachofanyika Jumapili hii huko Tripoli Libya.
Mwandishi:Aboubakary Liongo
Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman