Mawaziri Tanzania watakiwa kuheshimu mipaka yao ya madaraka
3 Oktoba 2022Rais Samia aliyetangaza mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri amewaapisha mawaziri hao katika hafla fupi iliyofanyika katika ikulu ya Dar es Salaam. Mabadiliko yaliyofanywa na rais huyo wa taifa hilo la Afrika Mashariki yamewashtua wengi. Samia amewaelekeza mawaziri hao kutambua kwamba jambo lolote wafanyalo lazima lihakikishe linafuata misingi ya katiba ya nchi.
Kwenye mabadiliko hayo, Rais Samia amemfuta kazi aliyekuwa waziri wa mambo ya nje, Leberata Mulamula na nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa, Stergomana Tax ambaye wakati fulani amewahi kuwa mtendaji mkuu wa jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC.
Wachambuzi wa mambo bado wanaendelea kukuna vichwa kujua sababu za kufutwa kazi kwa Balozi Mulamula na hata mwenyewe katika hotuba yake wakati akiwaapisha mawaziri hao, Rais Samia hakueleza lolote mbali ya kuwasisitizia kufanya kazi kwa utiifu.
Kuapishwa kwao kumeshuhudiwa na viongozi kadhaa wa kiserikali akiwamo spika wa bunge la Jamhuri, Dr Tulia Ackson.
Wengine walioapishwa leo, ni waziri Innocent Bashungwa ambaye sasa anakuwa waziri wa ulinzi na kujenga taifa, akitokea wizara ya tamisemi iliyokabidhiwa kwa Angela Kairuki ambaye pia ameteuliwa kuwa mbunge.
Mwandishi: George Njogopa