Mawaziri wa EU kujadili ufadhili wa Ukraine na mzozo wa Gaza
23 Oktoba 2023Kuhusu Mashariki ya Kati, swali kuu ni jinsi Umoja wa Ulaya unavyoweza kuzuia mzozo huo kutanuka zaidi.
Kuhusu Ukraine, wajumbe hao watahitajika kufafanua bayana katika miezi ijayo jinsi Umoja wa Ulaya utakavyopaswa kutekeleza mipango ya ahadi za kiusalama ambazo zimewekwa na nchi za Magharibi.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amependekeza ufadhili wa muda mrefu wa misaada ya kijeshi na pia kutumia fedha za Umoja wa Ulaya kusaidia katika kununua ndege za kivita za kisasa pamoja na makombora.
Hususan anataka kiasi cha dola bilioni 5.3 kutolewa kila mwaka kuanzia mwaka 2024 hadi mwisho wa mwaka 2027.
Mawaziri wa mambo ya nje wa EU wakutana mjini Kyiv nchini Ukraine
Mawaziri wa Uhamiaji wa EU wakutana kujadili usalama, uhamiaji
Hakuna makubaliano yanayotarajiwa kuwa na mabadiliko makubwa kuafikiwa kwenye mkutano huo wa Jumatatu. Tayari wanachama kadhaa wa Umoja wa Ulaya wameonesha kutokuwa tayari kuanzisha mpango mpya wa ufadhili wa muda mrefu kwa Ukraine.
Mitizamo tofauti ya wanachama kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati
Pia kuna mgawanyiko miongoni mwa nchi wanachama kuhusu tathmini ya hatua ya Israel baada ya shambulizi la kundi la Hamas dhidi yake mnamo Oktoba 7.
Kundi la Hamas limeorodheshwa na baadhi ya nchi ikiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya kuwa la kigaidi.
Kwa mfano viongozi wa Uhispania wanaishutumu Israel kwa kukiuka sheria ya kimataifa kufuatia wito wake kutaka baadhi ya wakaazi wa mji wa Gaza kuondoka katika baadhi ya maeneo. Aidha wanaunga mkono wito wa usitishaji vita.
Kwa upande mwingine, viongozi kutoka mataifa kama Ujerumani wanapinga msimamo huo, na wanasisitiza haki ya Israel kujilinda.
Mada nyingine inayotarajiwa kujadiliwa kwenye mkutano huo wa mawaziri ni mgogoro kati ya Armenia na Azerbaijan. Baada ya mkutano wao, watakuwa pia na mazungumzo na wawakilishi wa Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan.
Ukraine yasema imedungua droni 9 za Urusi
Wakati mgogoro wa Ukraine na Urusi ukiwa miongoni mwa ajenda kwenye meza ya mazungumzo, mzozo huo umeendelea kutokota.
Mapema leo, Ukraine imesema imezuia droni za Urusi zilizokusudia kufanya shambulizi kubwa usiku wa kuamkia leo katika jimbo la Bahari Nyeusi Odessa.
Gavana wa kijeshi, Oleh Kiper, ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Telegram kwamba mfumo wa ulinzi wa angani ulidungua ndege tisa zinazopeperushwa bila rubani.
Aliandika zaidi kwamba baadhi ya mabaki ya ndege zilizodunguliwa yalianguka kwenye jengo karibu na ufuo wa bahari na kusababisha moto, ambao tayari umeshazimwa.
Hakukuwa na taarifa za moja kwa moja ikiwa kulikuwa na watu waliouawa au waliojeruhiwa kutokana na mashambulizi hayo.
Kulingana na jeshi la Ukraine, jumla ya droni 14 na kombora moja vilidunguliwa kote nchini humo.
Ukraine imekuwa ikijitetea dhidi ya uvamizi mkubwa uliofanywa na Urusi kwa miezi 20 sasa.
Mara kwa mara, Urusi imekuwa ikiulenga mji wa bandari wa Odessa ambao ni muhimu katika usafirishaji wa nafaka za Ukraine.
Chanzo: DPAE