Mawaziri wa EU na AU-wazingatia uamuzi wa mahakama Congo
22 Januari 2019Wakiulizwa kuhusiana na uchaguzi wa hapo Desemba 30, viongozi wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wamesema kwamba wamejadiliana kuhusu matokeo ya uchaguzi huo katika mkutano wao mjini Brussels, wakidokeza kuhusu uungaji mkono wa mahakama kwa Tshisekedi. Maafisa hao katika mkutano na waandishi habari hawakusema wazi hadharani kwamba wanamtambua Tshisekedi kama mshindi , na hata hawakumpongeza.
"Tumezingatia tamko la mahakama ya katiba, changamoto ya rais mpya ni kubwa katika masuala mengi," mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa ulaya Federica Moghrini aliwaambia waandishi habari , akiwa pamoja na wajumbe wa Umoja wa Afrika.
"Tunafikiri yote haya yanahitaji kwamba rais ni lazima awe nguvu ya kuunganisha," Mogherini amewaambia waandishi habari, akisema Umoja wa Ulaya utaendelea kufanyakazi kwa karibu na Congo.
Tukotayari kufanyakazi na Congo
Waziri wa mambo ya kigeni wa Rwanda Richard Sezibera, ambaye anauwakilisha Umoja wa Afrika katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa makundi hayo ya mataifa , pia amesema amezingatia uamuzi huo wa mahakama.
"Umoja wa Afrika unatambua kwamba taasisi za jamhuri ya kidemokrasi ya Congo zimetangaza matokeo ya mwisho na unaendelea kuwa na dhamira ya kufanyakazi pamoja na watu wa Congo katika kuendelea kushughulikia changamoto ambazo zimebakia."
Kamishna wa Umoja wa Afrika anayehusika na masuala ya amani na usalama Smail Chergui, ambaye amezungumza baada ya Mogherini na Sezibera, amesema yuko tayari kufanyakazi na Tshisekedi pamoja na vyama vyote vya kisiasa nchini Congo lakini alikata kutoa maelezo zaidi.
Mahakama ya katiba ya Congo mapema siku ya Jumapili ilikataa malalamiko ya mshindi wa pili wa uchaguzi nchini humo Martin Fayulu kwamba uchaguzi umetendewa kinyume kwa kuunga mkono ushindi wa Tshisekedi, na upinzani dhidi ya uchaguzi huo unaonekana kulainika.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Daniel Gakuba