Mawaziri wa EU wajadili kulegeza vikwazo dhidi ya Syria
13 Januari 2025Hayo yamesemwa na mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Kaja Kallas.
Mwanadiplomasia huyo hata hivyo ameeleza kwamba, kulegezwa kwa vikwazo hivyo kutategemea viongozi wapya wa Syria kutekeleza mchakato wa mpito wa kisiasa unaojumuisha makundi yote baada ya kupinduliwa madarakani kwa Rais Bashar al-Assad.
Soma pia: Ujerumani kuhudhuria mkutano wa kimataifa juu ya Syria
Kauli ya Kallas ameitoa wakati wa mkutano wa wanadiplomasia wakuu wa Umoja wa Ulaya na Mashariki ya Kati uliofanyika katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh kujadili mustakabali wa Syria.
Saudi Arabia imetoa wito wa kuondolewa vikwazo ambavyo vinatishia kuzuia juhudi za Syria kujikwamua baada ya karibu miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya takriban watu 500,000 na kuwaacha nusu ya raia nchini humo bila ya makaazi rasmi.