Mawaziri wa Fedha wa G-7 waonya dhidi ya"Brexit"
21 Mei 2016Mawaziri wa Fedha kutoka kundi la nchi saba zenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani (G-7) wameonya kwamba kujitowa kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya kutazidisha ukosefu wa utulivu na kuharibu ukuaji wa uchumi duniani ikiwa umebaki mwezi mmoja kabla ya Uingereza kuamuwa juu ya suala hilo katika kura ya maoni.
Mawaziri hao wa fedha wamesema katika taarifa Jumamosi (21.05.216) wakati wa mkutano huko Sendai Japani kwamba "wakati mashaka juu ya hali ya dunia yamekuwa yakizidi kuongezeka kutokana na mizozo ya kisiasa ya kimaeneo,ugaidi na utitiri wa wakimbizi, fadhaa ya kutaka kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya nazidi kufanya hali ya kiuchumi duniani kuwa ngumu zaidi."
Ingawa mawaziri hao wamekuwa na msimamo mmoja katika kutaka Uingereza iendelee kubakia katika Umoja wa Ulaya wamekiri kwamba hawawezi kuanya kitu chochote ziada ya kuweka matumaini.
Waziri wa Fedha wa Ufaransa Michel Sapin ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba "Kundi la G-7 halikuzungumzia juu ya "Mpango B" kukabiliana na kile kitakachotokea iwapo Uingereza itajitowa Umoja wa Ulaya na kwamba tumezungumzia juu ya njia za kuisaidia Uingereza ibakie Umoja wa Ulaya."
Kura ya maoni
Suala la kura ya maoni kwa Uingereza kuamuwa iwapo ibakie au ijitowe Umoja wa Ulaya limekuwa suala muhimu kwa masoko ya dunia na watengeza sera ambao wanachoweza kufanya ni kusubiri tu na kuona kile watakachosema Waingereza katika kura hiyo ya maoni iliopangwa kufanyika tarehe 23 mwezi wa Juni.
Sapin hakufafanuwa hatua zozote zile ilizojadili kundi hilo la G-7 kuibakisha Uingereza katika Umoja wa Ulaya wakati wa mahojiano yake pembezoni mwa mkutano huo wa mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu katika mkoa wa Sendai ,kaskazini mashariki ya Japani.
Amesema "Brexit" yaani kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya kutakuwa na taathira kubwa sana kwamba kutaiathiri Uinigereza na Ulaya kwa sababu wawekezaji watakuwa na wasi wasi jambo ambalo litaathiri uingiaji wa mitaji.
Mawaziri hao wa fedha hawakuwa na la kufanya ziada ya kuunga mkono wito wa Waziri Mkuu wa Uingreza David Cameron kwa nchi hiyo yenye kushika nafasi ya pili kwa nguvu za kiuchumi barani Ulaya kuendelea kubakia Umoja wa Ulaya.
Wasi wasi wa pamoja
Waziri wa Fedha wa Canada Bill Morneau ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba "Tuna wasi wasi kweli kwa pamoja juu ya hatari ya kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya na tunaamini kwamba jambo hilo linaweza kuwa na taathira fulani za kiuchumi. Ameongeza kusema kwamba " hatujazungumzia hatua mahsusi ambazo yumkini zikachukuliwa kutokana na hali hiyo."
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble amesema nchi wanachama wa kundi la zimekubali kwamba "kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya utakuwa sio uamuzi sahihi" lakini amekiri kwamba hatima ya Uingereza katika umoja huo wa nchi wanachama 28 moja kwa moja itakuwa katika mikono ya wapiga kura wake.
Kampeni kali ya Cameron ya kuwavutia wale wenye mashaka na Umoja wa Ulaya kuunga mkono kuibakisha Uingereza katika umoja huo inaonekana kuanza kuzaa matunda kwa sasa.Paundi ya Uingereza wiki hii imefikia thamani ya juu kabisa dhidi ya euro kuwahi kufikia katika kipindi cha miezi mitatu na nusu wakati uchunguzi wa maoni ukionyesha kuimarika kwa uunganji mkono wa Umoja wa Ulaya.
Kampeni ya kuibakisha Uingereza
Uchunguzi huo umegunduwa kwamba asilimia 55 wanapendelea kubakia Umoja wa Ulaya dhidi ya asilimia 37 wanaotaka ijtowe.Hoja za kiuchumi zimeonekana kuwa na taathira fulani kwamba "Brexit" kujitowa kwa Uingereza kutasababisha machafuko ya masoko ya kifedha na kuuathiri uchumi wa Uingereza wenye thamani ya dola bilioni 2.9.
Lakini bado suala hilo linaonekana kuwa nyeti kwa wanasiasa kutoka nchi nyengine kutokana na kule matamshi yao kuja kuonekana nchini Uingereza kama vile yanaingilia kati masuala ya ndani ya nchi hiyo.Halmashauri ya Umoja wa Ulaya kwa kiasi kikubwa haikujiingiza katika kampeni hiyo.
Mawaziri wa fedha wa G- 7 wamekamilisha mkutano wao wa siku mbili Jumamosi nchini Japani ambapo ziada ya Uingereza kundi hili pia linazijumuisha nchi za Ujerumani, Ufararansa,Italia,Marekani, Japani na Canada.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP
Mhariri :Iddi Sessanga