1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa G7 wakutana kujadili mzozo wa Gaza na Ukraine

Daniel Gakuba
25 Novemba 2024

Wanadiplomasia wa ngazi za juu wa nchi za kidemokrasia zilizoendelea kiviwanda G7, wanakutana nje kidogo ya mji mkuu wa Italia, Roma, kujadili mizozo inayoitikisa dunia, ikiwemo vita vya Ukraine na vya mashariki ya kati.

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa kundi la G7.
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa kundi la G7 na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya wakiwa kwenye mkutano nchini Italia. Picha: Claudia Greco/REUTERS

Mkutano huo unafanyika chini ya kiwingu cha ushindi wa rais mteule wa Marekani, Donald Trump, ambaye anatarajiwa kuibadilisha pakubwa sera ya nje ya Marekani atakapochukua hatamu za uongozi mwanzoni mwa mwaka ujao.

Kwenye agenda ya mkutano huo unaoanza katika mji mdogo wa Fiuggi ulioko umbali wa takribani kilomita 80 mashariki mwa Roma, vita vya Ukraine na vya mashariki ya Kati vitapewa kipaumbele.

Lakini pia suala la kutolewa kwa waranti wa kukamatwa kwa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Yoav Gallant litakuwa kwenye meza ya mjadala.

Nchi zinazounda kundi la G7 ni Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Canada, Italia na Japan. Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi kadhaa ya Kiarabu, zikiwamo Saudi Arabia, Misri, Jordan, Umoja wa Falma za Kiarabu na Qatar wamealikwa katika mazungumzo hayo, na pia katibu mkuu wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu.

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Italia Enzo Moavero Milanesi ameviambia vyombo vya habari mjini Fiuggi, kuwa kwa kuzingatia mazingira ya dunia ya sasa, mkutano huu umefanyika kwa muda muafaka.

‘‘Dunia ya sasa imo hatarini na imejaa matatizo; mizozo ya Ukraine na Mashariki ya Kati imezua uhasama na vitisho ambavyo vinashuhudiwa kila siku ulimwenguni kote. Kwa hiyo ni muhimu kuwa nchi za magharibi zinashirikiana kwa karibu na kuwa na mtazamo mmoja, na kutoa aina fulani ya hakikisho la kuelekea kwenye dunia bora na yenye utulivu.‘‘

Mawaziri wa kiarabu waalikwa kujadili mzozo wa kanda ya mashariki ya kati 

Kualikwa kwa mataifa ya kiarabu, amesema Waziri wa sasa wa Italia Antonio Tajani, kunalenga kushirikisha mawazo yao katika juhudi za kupunguza uhasama katika ukanda wa mashariki ya kati.

Zitajadiliwa hatua za kumaliza mapigano katika Ukanda wa Gaza, na utawala mpya utakaowekwa baadaye, na pia mipango ya ukarabati baada ya vita kumalizika.

Siku ya pili ya mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za G7 itajikita katika vita vya Ukraine, na yatahudhuriwa na Waziri wa mambo ya nchi wan chi hiyo Andriy Sybiga.

Mizozo mingine inayotarajiwa kutupiwa jicho na mawaziri hao ni ile ya Haiti, Sudan na hali ya mambo nchini Venezuela.

Huu utakuwa mkutano wa mwisho wa aina hii kwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken kabla ya mabadiliko ya utawala mjini Washington mwanzoni mwa mwaka ujao wa 2025.

Kuna hofu kuwa utawala mpya wa Rais Donald Trump utaifanyia mageuzi makubwa sera ya Marekani kuhusu Ukraine, na utaeipendelea zaidi Israel dhidi ya Wapalestina.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW