Mawaziri wa kanda ya Euro na sehemu ya pili ya mkopo kwa Ugiriki
13 Machi 2012Palihitajika muda wa miezi kadhaa,lakini sasa fungu la pili la msaada kwa Ugiriki limeshapatikana.Ridhaa ya mataifa wanachama wa kanda ya Euro hapo kesho ni utaratibu wa kawaida tu.Hata hivyo lakini kanda ya Euro inakabiliwa na kishindo chengine: Hispania.Serikali ya mjini Madrid inalazimika kuzidi kufunga mkaja ili kudhibiti nakisi ya bajeti yake.
Mawaziri wa fedha wa kanda ya Euro wameonekana wamepumua kidogo.Mgogoro mkubwa wa Ugiriki unaonyesha kufumbuliwa ,angalao kwa sasa.Masharti ya kutolewa fungu la pili la msaada yamekamilika,alisema mkuu wa kundi la mataifa wanachama wa kanda ya Euro,Jean-Claude Juncker,hata kabla ya kuwasili mjini Brussels hapo jana.
"Hakuna shaka yoyote,fungu la pili la msaada kwa Ugiriki litaidhinishwa na litatolewa."Amesema.
Hata hivyo uamuzi wa mwisho utafikiwa kesho jumatano,
Ugiriki inatarajiwa kupatiwa zaidi ya Euro bilioni 100.Miongoni mwa masharti ya kutolewa fungu hilo la pili ni pamoja na sekta ya kibinafsi kusamehe sehemu kubwa ya madeni yake.Yamepindukia makadirio.Hadi mwaka 2020 nchi hiyo itapunguza kiwango cha madeni yake hadi asili mia 117 ya pato la ndani.Hapo awali watu walikuwa wakizungumzia kiwango cha asilimia 120.
Asili mia 96 ya wafadhili wamesharidhia hadi wakati huu anasema waziri wa fedha wa Ugiriki Evangelos Venizelos.Anasema anataraji na waliosalia pia wataridhia.
Njia bado ni ndefu hadi Ugiriki itakapoweza kujitegemea wenyewe.Na hadi wakati huo utakapowadia nchi za kanda ya Euro zinaonyesha kukabiliana na kishindo chengine;Hispania.Mwaka jana nchi hiyo ilikabwa na nakisi ya bajeti iliyofikia asili mia 8.5 ya pato lake la ndani.Mwaka huu halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imeamuru nakisi ya bajeti ya Hispania isipindukie asili mia 4.4,lakini serikali ya mjini Madrid inategemea itafikia asili mia 5.8.Lakini hali hiyo haimridhishi yeyote,si wanachama wa Umoja wa Ulaya na wala si halmashauri kuu ya Umoja huo.Kamishna wa masuala ya sarafu Olli Rehn amesema wakati wa mkutano na waandishi habari jana usiku:"Msimamo wa kanda ya Euro ambao halmashauri kuu inauunga mkono moja kwa moja ni kwamba serikali ya Hispania inaweza kupindukia marekebisho ya nakisi yaliyokwishatangazwa kwa asili mia 0.5 tu.
Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Wolfgang Schäuble haamini lakini kama mgogoro wa Hispania utafikia kipeo kama kile cha Ugiriki.
Mwandishi: Christoph Hasselbach/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Khelef