Mawaziri wa kigeni wa EU waitembelea Bucha
31 Machi 2026
Ziara hiyo inakusudia kuadhimisha miaka minne tangu wilaya hiyo ya mji mkuu wa Ukraine, Kiev, kukombolewa kutoka mikononi mwa wanajeshi wa Urusi na kuibuwa ukatili mkubwa wa kivita uliotendeka.
Bucha, iliyo magharibi mwa Kiev, ilikaliwa na vikosi vya Urusi katika siku za mwanzo za vita vilivyoanzishwa na Urusi mnamo Februari 2022.
Baada ya wanajeshi wa Ukraine kufanikiwa kukirejesha mikononi mwao, miili ya raia ilikutikana imetapakaa kwenye mitaa ya kitongoji hicho, huku ikiwa imefungwa mikono kwa nyuma.
Haraka, Bucha ikageuka kuwa alama ya uhalifu wa vita hivyo, na baadaye Umoja wa Mataifa ulithibitisha vifo vya mamia ya raia.
Maafisa wa Urusi wanaendelea kukanusha tuhuma za mauaji hayo na badala yake wanadai ukatili wa Bucha lilikuwa tukio lililobuniwa na Ukraine yenyewe.