Mawaziri wa kigeni wa UAE, Israel kufanya mazungumzo Berlin
6 Oktoba 2020Wakati huo huo balozi wa Ujerumani nchini Belarus Manfred Huterer, ameondoka kwa muda nchini humo, kwa mujibu wa vyanzo katika ofisi ya wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani kabla ya mkutano wa kansela Angela Merkel na kiongozi wa upinzani nchini humo, Slevtlana Tikhanovslaya.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel Gabi Ashkenazi na mwenzake wa UAE Sheikh Abdullah bin Zayed al-Nahyan walisalimiana kwa kugusana viwiko vya mkono ikiwa ni hatua za kujikinga na virusi vya corona, wakati walipokutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza baada ya nchi zao, ambazo hapo zamani zilikuwa mahasimu wakubwa, kutia saini makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani katikakti ya mwezi Septemba kurejesha uhusiano wao wa kibalozi.
Wakiambatana na mwenyeji wao, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas, mawaziri hao wawili walitembea katika eneo hilo la kumbukumbu, lililo la matofali makubwa ya saruji 2,700 yaliyowekwa katika eneo ambalo ni sawa na viwanja vitatu vya mpira.
Ni kumbukumbu ya Wayahudi milioni sita waliouwawa na utawala wa kinazi wa Adolf Hitler.
Ziara hiyo ya Sheikh Abdullah katika kumbukumbu ya Holocaust ni hatua ya kiishara tu, ikionesha kubadilka kwa mtazamo katika mataifa ya Kiarabu kuelekea Israel na wayahudi.
Mizozo ya kisiasa imesababisha hali mbaya ya wasi wasi kati ya dini ya Kiislam na ya Kiyahudi pamoja na kukana kutokea holocaust kitu ambacho kimekuwapo kwa kiasi kikubwa katika mataifa mengi ya Kiarabu.
Maas aliita ziara hiyo kuwa ni heshima kubwa ambayo wizara za mambo ya kigeni ya Israel na Emirati zimeipatia Ujerumani kama sehemu kwa ajili ya mkutano wao wa kwanza wa kihistoria.
Wakati hayo yakitokea balozi wa Ujerumani nchini Belarus Manfred Huterer, ameondoka kwa muda nchini humo, kwa mujibu wa chanzo katika ofisi ya waziri wa mambo ya kigeni ya Ujerumani mjini Berlin.
Huterer aliondoka , "ili kuongoza majadiliano mjini Berlin" kwa misingi ya mshikamano na Poland na Lithuania, ofisi hiyo imesema.
Poland na Lithuania zimewaita nyumbani mabalozi wake nchini Belarus kwa ajili ya mashauriano kufuatia madai ya Belarus kwamba nchi hizo zipunguze uwepo wa wanadiplomasia wao nchini humo, waziri wa mambo ya kigeni wa Lithuania Linas Linkevicius alisema katika taarifa mapema leo.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajiwa kukutana na kiongozi wa upinzani wa Belarus anayeishi uhamishoni Svetlana Tikhanovskaya kwa mazungumzo mjini Berlin leo, wakati maandamano makubwa yanaendelea nchini Belarus dhidi ya rais Alexander Lukashenko kurejea madarakani.