1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa G7 wakutana ana kwa ana

3 Mei 2021

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken ameyafungua rasmi mazungumzo ya ana kwa ana ya mawaziri wa kundi la mataifa saba ya G7 kwa kuwasilisha mkakati mpya wa serikali yake kuelekea Korea Kaskazini,

London G7-Außenminister-Treffen
Picha: Ben Stansall/AFP/AP/picture alliance

Mkutano huu ni wa maandalizi ya mkutano wa kilele wa G7 utakaohudhuriwa na rais Joe Biden wa Marekani, utakaofanyika nchini Uingereza mwezi ujao na ikiwa ni safari ya kwanza ya nje tangu alipoingia madarakani mwezi Januari, ukilenga kurejesha upya mahusiano na washirika wa jadi wa Marekani baada ya zama za migawanyiko chini ya utawala wa Donald Trump.

Mawaziri wa mambo ya kigeni na uchumi kutoka kundi hilo la mataifa 7 tajiri zaidi ulimwenguni, G7 wanakutana ana kwa ana wiki hii jijini London baada ya miaka miwili, na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken atafanya mazungumzo na mwenzake wa Uingereza ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo, Dominic Raab.

Masuala yanayotarajiwa kutawala mazungumzo kati ya Blinken na Raab ni kuondoka kwa wanajeshi wa kigeni nchini Afghanistan na mazungumzo ya baada ya Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya "Brexit". Suala la uwezekano wa kubadilishana wafungwa na Iran pia huenda likajadiliwa kwenye mazungumzo hayo, wakati uvumi ukisambaa kwamba wanajadiliana kubadilishana wafungwa na miongoni mwao akiwa ni mwanaharakati raia wa Uingereza na Iran Nazanin Zaghari-Ratcliffe.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Dominic Raab akimkaribisha BlinkenPicha: Ben Stansall/AFP/AP/picture alliance

Mapema leo, Blinken alifanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Japan Toshimitsu Motegi, wakigusia masuala kadhaa ambayo ni pamoja na janga la virusi vya corona na mzozo wa kimazingira pamoja na kuongezeka wasiwasi kufuatia mipango ya nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini na kukubaliana kushirikiana katika mkakati wa kuondoa shughuli za kijeshi katika rasi ya Korea.

Aidha waliugusia mzozo unaoendelea kufukuta nchini Myanmar, na kwa pamoja walijadiliana umuhimu wa kulisaidia taifa hilo kurejea kwenye kidemokrasia na kuuwajibisha utawala wa kijeshi ulioiangusha serikali ya kiraia katika mapinduzi ya Februari Mosi.

Kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Marekani, ziara hii ya Blinken jijini London pia itagubikwa na mazungumzo magumu kuhusu Urusi, Ukraine, Iran na changamoto ya kiulimwengu inayoletwa na China.

India, Korea Kusini, Afrika Kusini na mwenyekiti wa Jumuiya ya nchi za kusini Mashariki mwa Asia ASEAN, Brunei yamealikwa kwenye mkutano huo, utakaowakutanisha mawaziri wote wa mataifa hayo ya G7 hapo kesho.

Kutoka London, Blinken anatarajiwa kwenda Kyiv, wakati hofu ikiongezeka kuhusiana na mahusiano kati ya Marekani na Ukraine, na hasa kufuatia hoja mpya zinazotolewa na Marekani kuhusiana na lengo la Urusi nchini humo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW