1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa mambo ya nje Urusi na Ukraine wakutana Uturuki

Hawa Bihoga
10 Machi 2022

Mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na Ukraine wameanza mkutano wao wa kujadili njia za kumaliza vita nchini Ukraine.

Türkei | Kuleba, Lawrow, Cavusoglu - Außenministertreffen in Antalya
Picha: Cem Ozdel/AA/picture alliance

Hii ni mara ya kwanza kwa wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Urusi na Ukraine kukutana tangu Urusi ilipovamia kijeshi Ukraine zaidi ya wiki mbili sasa.

Mkutano kati ya Sergey Lavrov wa Urusi na Dmotry Kuleba wa Ukraine unafanyika ikiwa tayari kumekuwepo na miito kutoka jumuia mbalimbali ya kusitisha mapigano huko Ukraine.

Mwenyeji wa mazungumzo hayo waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu ambae anashiriki mazungumzo hayo ya amani amesema, dima ya mkutano huo ni kuandaa mazungumzo kati ya marais wa mataifa hayo mawili ambayo yataongozwa na Rais wa Ururuki.

Soma zaidi: Ukraine yajaribu kuwasajili wapiganaji wa kiafrika

Aidha, Kuleba amependekeza kuwepo kwa mazungumzo ya bayana kati ya Rais Volodmiry Zelensky wa Ukraine na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin.

Licha ya jumuia ya kimataifa kuendeleza jitihada za kuzima mzozo huo Uturuki nayo kwa majumaa kadhaa sasa imechukua jukumu la upatanishi baina ya pande hizo mbili lakini wachambuzi wanahofia kuna uwezekano mdogo wa mafanikio katika mazungumzo hayo.

Wachambuzi hawaoni tumaini kwenye mazungumzo hayo ya Uturuki

Mazungumzo ya hapo awali yalilenga zaidi kuunda eneo dogo la kusitisha mapigano ili kuwafikia raia katika miji iliyozingirwa, haswa Mariupol, bandari ya kusini ambapo mamia ya maelfu ya watu wamenaswa bila kupata maji, dawa au chakula.

Mawaziri wa mambo ya nje Urusi, Uturuki na UkrainePicha: Sergei Ilnitsky/Fatih Aktas/Lev Radin/picture alliance

Ukraine imesema Urusi imekuwa ikitekeleza kile ilichokiita mauaji ya halaiki kwa kuishambulia hospitali ya watoto hapo jana Jumatano.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urusi Maria Zakharova amekanusha madai hayo ya Ukraine kwa kusema kuwa habari hizo zinatishia usalama wa taifa hilo.

Soma zaidi:Urusi yashambulia hospitali tatu Ukraine

Hata hivyo ikulu ya Urusi, Kemlin imesema kuwa itawasiliana na jeshi la Urusi kuthibitisha madai hayo ya kulipua hospitali ya watoto katika mji uliozingirwa wa Mariupol.

IOM: Idadi ya wanaokimbia Ukraine yaongezeka

Wakati hayo yakiendelea shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamaji, IOM kupitia tovuti yake limesema kuwa haki kufikia leo  kiasi cha watu milioni 2.3 wamekimbia Ukraine, ambapo takribani watu 112,000 ni kutoka mataifa mengine.

Wagonjwa wa Ukraine wakimbilia Poland

01:39

This browser does not support the video element.

Katika hatua nyingine viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo katika mkutano usio rasmi wa kilele huko Ufaransa baada ya wiki mbili za kuhangaika kusambaza silaha, kuwahifadhi karibu watu milioni 2 na kusainiwa kwa awamu tatu za vikwazo vikubwa dhidi ya Urusi kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.

Soma zaidi:Mapigano yasitishwa Ukraine kuruhusu raia kuondoka

Viongozi hao pia wanatarajia kujadili hatua zaidi za kusaidia nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zilizo karibu na Ukraine ambazo zimewapokea maelfu ya watu wanaokimbia vita.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW