1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Mawaziri wa mambo ya nje wa G20 wakutana Brazil

21 Februari 2024

Mawaziri wa mambo ya nje wa Kundi la nchi zilizostawi kiviwanda duniani - G20 wanaanza leo mkutano wa siku mbili nchini Brazil, huku mizozo ya vita vya Gaza na Ukraine ikitarajiwa kuwa mada kuu.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov
Mkutano wa G20 mjini Rio de Janeiro utagubikwa na mizozo ya Israel na Hamas na vita Urusi nchini UkrainePicha: Stefani Reynolds/AP Photo/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov wapo mjini Rio de Janeiro kuhudhuria mkutano huo wa kwanza wa ngazi ya juu wa G20 mwaka huu.

Mwanadiplomasia mkuu wa China Wang Yi hatohudhuria. Brazil, ambayo ilichukua urais wa kupokezana wa G20 kutoka kwa India Desemba mwaka jana, imeelezea matumaini ya kile Rais Luiz Inacio Lula da Silva anachokiita "jukwaa lenye uwezo mkubwa zaidi wa kushawishi ajenda ya kimataifa kwa njia chanya."

Lakini mwishoni mwa wiki akiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika, Lula alianzisha mgogoro wa kidiplomasia kwa kuituhumu Israel kuwa inafanya "mauaji ya halaiki", akiilinganisha operesheni yake ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza na maangamizi yaliyofanywa dhidi Wayahudi.