1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

G20 yaunga mkono suluhu ya mataifa mawili kwa mzozo wa Gaza

23 Februari 2024

Brazil imesema kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la G20 wanaunga mkono suluhisho la mataifa mawili kwa mzozo kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza

Waziri wa mambo ya nje wa Brazil  Mauro Vieira akiwahutubia waandishi habari baada ya kukamilika kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G20 mjini Rio de Janeiro, Brazil, mnamo Februari 22, 2024
Waziri wa mambo ya nje wa Brazil Mauro VieiraPicha: Mauro Pimentel/AFP/Getty Images

Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya bunge la Israel kupinga kwa wingi wa kura utambuzi wowote wa upande mmoja wa taifa la Palestina, katika hatua ambayo waziri mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu amesema imetuma ujumbe mzito kwa jumuiya ya kimataifa.

Mawaziri wa G20 wakubaliana kwa pamoja kuhusu suluhisho la mataifa mawili

Waziri wa mambo ya nje wa Brazil Mauro Vieira, amewaambia waandishi habari kwamba kulikuwa na makubaliano ya pamoja kwa suluhisho la mataifa mawili kama la kipekee katika mzozo huo wa Mashariki ya Kati.

Borrell asisitiza kuhusu makubaliano ya suluhisho la mataifa mawili

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alikuwa amemtaka Vieira kutumia hotuba yake ya mwisho kwenye mkutano huo kuuelezea ulimwengu kwamba katika mkutano huo wa G20, kila mtu alikuwa anaunga mkono suluhisho hilo la mataifa mawili kwa kuweko kwa taifa huru la Palestina pamoja na lile la Israel.

Soma pia:Juhudi mpya zaanzishwa ili kusitisha mapigano Gaza

Vieira amesema mataifa mengine katika mkutano huo pia yamekariri ukosoaji wao dhidi ya vita vya Urusi nchini Ukraine lakini kulikuwa na dalili ndogo za ufanisi wa kidiplomasia.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep BorrellPicha: YVES HERMAN/REUTERS

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, ameyashtumu mataifa ya Magharibi kwa ukosoaji wake kuhusiana na kifo cha kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny katika gereza moja nchini humo siku ya Ijumaa iliyopita.

Soma pia:Mawaziri wa G20 waikosoa uvamizi wa Urusi, Ukraine

Lavrov amewaambia waandishi habari pembezoni mwa mkutano huo wa G20 kwamba mataifa hayo yanajifanya kama waendesha mashtaka, walalamikaji na majaji na kuongeza kuwa hayana haki ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Blinken ashinikiza kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa Haiti

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, ameshinikiza kuendelezwa kwa mipango iliyochelewa ya kutuma kikosi cha kimataifa kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Haiti kusaidia katika kukabiliana na magenge ya wahalifu.

Soma pia;Mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la G20 wakutana Brazil

Katika kikao kilichoandaliwa pembezoni mwa mkutano huo wa G20 na kuhudhuriwa na waakilishi kutoka Canada, Kenya , Haiti na Umoja wa Mataifa miongoni mwa wengine, Blinken amesema kuwa ni salama kusema kuwa moja ya changamoto za dharura zinazoikabili jamii ya kimataifa iko nchini Haiti.

Masuala katika agenda ya mkutano wa G20 nchini Brazil

Kampeni ya kijeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza ilikuwa agenda kuu ya mkutano huo wa siku mbili pamoja na vita vya Urusi nchini Ukraine na kushindwa kwa Umoja wa mataifa na taasisi nyingine za kimataifa katika kukabiliana na migogoro.