1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa kigeni wa Marekani na Uingereza ziarani Kiev

11 Septemba 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na mwenzake wa Uingereza David Lammy wamewasili mjini Kiev katika ziara ya pamoja nchini Ukraine.

 Antony Blinken - David Lammy
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Lammy na mwenzake wa Marekani Antony Blinken Picha: Mark Schiefelbein/picture alliance/AP

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na mwenzake wa Uingereza David Lammy wamewasili mjini Kiev katika ziara ya pamoja nchini Ukraine, wakati nchi hiyo ikizidi kuzishinikiza nchi za Magharibi kuiruhusu kutumia makombora ya masafa marefu kuishambulia Urusi.

Waziri mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal jana kwenye mkutano na waandishi habari mjini Kiev alisema wataendelea kuzishinikiza nchi za Magharibi kila siku kuhusu suala hilo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alisafiri kwenda Kiev akitokea Londonambako aliituhumu Iran kwamba inaipelekea Urusi makombora ya kisasa ya masafa mafupi ya Fath-360 na kuitaja hatua hiyo kama kitendo cha kutisha cha kutanuwa vita.

Iran imekanusha tuhuma hizo na imeapa kuchukuwa hatua kujibu vikwazo vipya vilivyotangazwa na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusiana na suala hilo. Ziara ya Blinken na mwenzake wa Uingereza David Lammy mjini Kiev inafanyika wakati waziri mkuu Keir Starmer akitarajiwa kukutana na Rais Joe Biden Ijumaa wiki hii, katika ikulu ya White House.