1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa nje wa G20 kuanza mazungumzo, Bali

7 Julai 2022

Mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la mataifa ya G20 wamekusanyika katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia ka mazungumzo yanayotarajiwa kugubikwa na kiwingu cha vita vya Ukraine kesho Ijumaa.

Indonesien | G20 Treffen Bali
Picha: Russian Foreign Ministry Press Service/AP Photo/picture alliance

Kuelekea mazungumzo hayo kesho Ijumaa, (8.7.2022) mawaziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi na wa Urusi Sergey Lavrov wakiwa njiani kuelekea Bali, walionyesha kupuzia mbali kiwingu kilichogubika mkutano huo na kwanza walizuru mataifa kadha wa kadha ya Asia wakipigia debe uungwaji mkono lakini pia kuimarisha ushirikiano na mataifa ya ukanda huo. Imearifiwa mapema leo mawaziri hao walikutana mjini Bali, ambapo Lavrov alimuarifu Yi kuhusiana na utekelezaji na lengo la operesheni maalumu ya kijeshi nchini Ukraine, hii ikiwa ni kulingana na wizara ya mambo ya kigeni Urusi. Na baadaye waziri Yi akasisitiza:

Yi alisema, "Tuko tayari kufanya kazi na marafiki wa Urusi na kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuendeleza ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu kwa haki na ubora wa ulimwengu ujao".

Lavrov aidha mapema leo amekutana na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu na kujadiliana vita vya Ukraine, usalama wa chakula na hatua zilizopigwa kwenye mazungumzo ya amani nchini Syria.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken anawasili leo Bali na wizara ya mambo ya kigeni imesema hatakutana na Lavrov, lakini atazungumza na Wang Yi, siku ya Jumamosi.

Rais Joko Widodo(Kushoto) ana kibarua kigumu kuandaa mkutano wa kilele wa G20 mwishoni mwa mwaka, baada ya Marekani kutishia kususia iwapo Urusi itashiriki.Picha: MIKHAIL KLIMENTYEV/Sputnik/AFP

Marekani pamoja na washirika wake wamekuwa wakisaka namna ya kumuadhibu rais wa Urusi Vladimir Putin ikiwa ni pamoja na kutishia kususia mkutano wa kilele wa G20 utakaofanyika Bali mwezi Novemba, hadi Putin atakapoondolewa ushiriki kwenye jukwaa hilo. Ni kwa maana hiyo basi, rais Joko Widodo wa Indonesia atalazimika kuchukua jukumu kubwa na muhimu zaidi ya kuwa mwenyeji tu wa mkutano huo wa kilele.

Taifa hilo limekuwa likijitenga na kuegamia upande wowote kwenye mzozo wa Ukraine. Rais Widodo amekuwa kiongozi wa mwanzo kutoka bara la Asia kuzuru Urusi na Ukraine. Ingawa Ukraine si mwanachama wa G20, lakini Widodo amemwalika rais Volodymyr Zelensky kwenye mkutano huo wa Novemba, pamoja na rais Vladimir Putin akiwa na matumaini ya kuzituliza pande zote. Hata hivyo Zelensky amekwishasema atashiriki kwa njia ya video uwapo vita vitakuwa vikiendelea nchini mwake.

Imeripotiwa kwamba, Widodo alimueleza waziri mkuu wa Italia Mario Draghi pembezoni mwa mkutano wa kundi la mjini Berlin Ujerumani kwamba hata Putin hatahudhuria, ingawa Moscow imesema bado hawajafanya maamuzi. Hali hii inawaweka mawaziri hawa kwenye mtihani mzito hapo kesho wanapokutana kuanza maandalizi ya mkutano huo wa 17 kilele.

G7 kuisaidia zaidi Ukraine, kuishinikiza zaidi Urusi

This browser does not support the audio element.

Lengo kuu la mazungumzo ya kesho ni kuangazia namna ya kuboresha usalama wa chakula katika kipindi cha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, ambapo kunashuhudiwa kupanda kwa bei za vyakula na mafuta.

Mawaziri kutoka Argentina, Australia, Brazil, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Italia, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Korea Kusini, Uturuki, Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya wanakutana kwenye mkutano huo.

Mashirika: APE/AFPE/RTRE