1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Uhamiaji wa EU wajadili usalama na uhamiaji

Angela Mdungu
19 Oktoba 2023

Mawaziri wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo mjini Brussels kujadili namna ya kuboresha usalama wa mataifa yao baada ya kutokea kwa mashambulizi yaliyosababisha vifo katika nchi za Ubelgiji na Ufaransa.

EU-Ungarn | Sitz der EU-Kommission in Brüssel
Picha: Yves Herman/REUTERS

Mawaziri hao watajadili pia kuhusu wasiwasi uliotanda wa uwezekano wa watu kulazimika kuyahama makazi yao kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas huko Mashariki ya kati.

Umoja wa Ulaya wenye wanachama 27, tayari umeshatoa wito wa kuimarishwa kwa mipaka na kuwarejesha makwao raia wa kigeni. Pia umeshaingia makubaliano mapya na nchi za Afrika ya kuwazuia wakimbizi na wahamiaji wasiingie Ulaya tangu mwalimu mmoja aliposhambuliwa na kuuwawa Ufaransa na tukio la muomba hifadhi mmoja raia wa Tunisia kuwashambulia na kuwauwa watu wawili Jumatatu wiki hii mjini Brussels.

Kutokana na tukio hilo waziri mkuu wa Ubelgiji, Alexander De Croo alitoa wito wa hatua kali hasa za kuimarisha mipaka

Akizungumzia hali ya uhamiaji barani Ulaya makamu wa Rais wa Kamisheni ya Ulaya Margatitis Schinas kabla ya mkutano amesema mapema leo kuwa sheria zilizopo kuhusu kurejeshwa kwa wahamiaji haramu kwenye mataifa yao, hazijitoshelezi. Ameeleza kuwa kwa sasa mapendekezo mapya yanatazamiwa kujadiliwa wakati wa mkutano wa leo wa mawaziri wa uhamiaji.

Umoja wa Ulaya umekuwa ukihofia kuhusu ongezeko la wahamiaji tangu wakimbizi takribani milioni moja kutoka Syria walipoingia Ulaya kutokana na vita mnamo mwaka 2015.

Wahamiaji kutoka Afrika wakiwasili Ulaya katika Pwani ya kisiwa cha El Hiero, UhispaniaPicha: Europa Press/AP/picture alliance

Shambulio la mjini Brussels limedhihirisha kushindwa kwa mifumo ya uhamiaji na ya uombaji hifadhi katika Umoja huo, ikiwemo kuwepo kwa mianya ya kiusalama.

Soma zaidi: Viongozi wa Umoja wa Ulaya kujadili uhamiaji

Kumekuwepo pia na msukumo mpya wa kuingia mikataba na mataifa ya Afrika yakiwemo Misri na Moroko wa kuyapa misaada kwa sharti la kuwazuia wahamiaji wanaotaka kuingia Ulaya, sawa na mkataba wa hivi karibuni ambao Umoja huo uliiingia na Tunisia.

Umoja wa Ulaya ambao mataifa yake wanachama yana wakaazi wasiopungua milioni 450 umerekodi kuwa takribani watu 250,000 wamewasili mwaka huu kinyume cha sheria wakisaidiwa na walanguzi kwa kiasi kikubwa. Mwaka uliopita, Umoja wa Ulaya uliwahifadhi mamilion ya wakimbizi waliotokana na vita nchini Ukraine.