Mawaziri wa Ulaya wajadili mapendekezo ya Brexit
20 Julai 2018Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wanajiuliza maswali kuhusiana na waraka huo uliowasilishwa na serikali ya Uingereza.
Mawaziri hao wa Umoja wa Ulaya walijadili leo mianya iliyopo katika majadiliano ya Brexit na Uingereza wakati mjumbe wa Ujerumani akikiri kwamba ana wasi wasi kwamba muda unayoyoma kabla ya kupata makubaliano. Kiongozi wa majadiliano ya Brexit wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier alitarajiwa kuwafahamisha mawaziri hao kuhusu mazungumzo aliyofanya na mjumbe mpya wa Uingereza Dominic Raab, baada ya mkutano wao wa kwanza jana Alhamis.
Mapendekezo ya Uingereza yanaangalia kuhusu eneo la biashara huru la pamoja kwa ajili ya chakula, ambalo litashuhudia nchi hiyo ikikubali viwango vya Umoja wa Ulaya, huku ikikubali taratibu mbali mbali kuhusu huduma ambazo zitaruhusu Uingereza kuweka sheria kwa ajili ya sekta kama sekta yake kubwa ya masoko ya fedha.
Hata hivyo , Umoja wa Ulaya umekuwa kila wakati ukisisitiza kwamba Uingereza haitaweza kuchagua miongoni mwa uhuru wa kundi hilo la mataifa: ikiwa ni pamoja na uhuru wa kusafirisha bidhaa, huduma, watu na mitaji.
Makubaliano ya kujitoa EU
Mawaziri hawakutarajiwa kuidhinisha jibu lisilokuwa rasmi leo kuhusiana na waraka huo wa Uingereza, ambapo wanadiplomasia wa Umoja huo waliyaeleza mapendekezo hayo kuwa ni waraka mmoja miongoni mwa mingi. Waziri wa Ufaransa anayehusika na masuala ya Umoja wa Ulaya Nathalie Loiseau akizungumzia kuhusu mkutano huo alisema.
"Leo umuhimu wa kwanza ni kufanyia kazi makubaliano ya kujitoa. Tunapaswa kuwa tayari mwezi Oktoba kuidhinisha makubaliano ya kujitoa kwasababu baada ya hapo yanapaswa kuidhinishwa nchini Uingereza na tunapaswa kuyaidhinisha katika bunge la Ulaya. Kwa hiyo huo ndio umuhimu. Na natarajia kusikia kile ambacho Michel Barnier atakachotuambia juu ya kikao cha majadiliano."
EU imeweka mtazamo wake kuhusu mahusiano ya baadaye mapema mwaka huu. Waziri wa masuala ya Umoja wa Ulaya wa Ujerumani , Michael Roth , alisema waraka huo unakwenda kinyume na miongozo ya majadiliano ya Umoja wa Ulaya. Lakini miongozo hiyo sio msahafu," amewaambia waandishi habari kabla ya mazungumzo hayo leo. "Kuna sheria, na sheria hizi zinapaswa kufuatwa," waziri wa mambo ya kigeni wa Luxembourg Jean Asselborn alisema. "Hatupaswi kuzichezea. Kuna mamia kwa maelfu ya ajira hapa, au zaidi. Na kwa hali hii inahusu uthabiti barani Ulaya," ameongeza.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga