Umoja wa Ulaya waupitia mpango wa ulinzi wa Ukraine
30 Agosti 2023Mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya wamekutana katika mji wa Toledo, nchini Uhispania siku ya Jumatano katika eneo ambalo hapo zamani lilikuwa kiwanda cha silaha na sasa limegeuzwa kuwa chuo kikuu. Mawaziri hao wa ulinzi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanazingatia msaada wa fedha wa muda mrefu kwa jeshi la Ukraine.
Mawaziri hao wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell aliyependekeza mpango wa kupatikana kiasi cha euro bilioni 20 ambapo euro bilioni 5 kwa mwaka ziwe zinatolewa kwa ajili ya programu za silaha na mafunzo kwa Ukraine kwa kipindi cha mwaka 2024 hadi mwaka 2027. Lengo la mpango huo wa Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ni kusogeza karibu zaidi msaada wa kijeshi wa Umoja wa Ulaya kwa Ukraine tofauti na muundo ulio mbali wa malipo tofauti.
Soma:Mashambulizi ya droni ya Ukraine dhidi ya Moscow yanaweza kuongezeka
Mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya pia wanajadili masuala mapana juu ya kuiunga mkono Ukraine katika kujilinda dhidi ya uchokozi wa Urusi, pamoja na mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuwasilisha makombora milioni moja kabla ya mwisho wa mwaka huu wa 2023.
Wakati hayo yakiendeelea waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov na mwenzake wa Uturuki, Hakan Fidan, wanatarajiwa kujadili matayarisho ya mkutano kati ya marais wa nchi hizo mbili mjini Moscow siku ya Alhamisi.
Migogoro ya Ukraine, Syria, Libya na eneo kati ya Bahari Nyeusi na Bahari ya Caspian pia litakuwemo kwenye ajenda ya mawaziri hao pamoja na nishati hayo ni kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amethibitisha kwamba Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, atakutana na na Rais Vladimir Putin nchini Urusi hivi karibuni.
Ripoti za vyombo vya habari zinasema viongozi hao wawili wanaweza kukutana Septemba 4 katika mji wa pwani wa mapumziko wa Sochi. Putin na Erdogan wanatarajiwa pia kujadili mkataba wa nafaka katika Bahari Nyeusi, uliosimamishwa na Putin mnamo mwezi Julai.
Ukraine ni mojawapo ya wauzaji wakubwa wa nafaka duniani na usafirishaji wa nafaka kutoka nchi hiyo ni muhimu kwa kuleta utulivu wa bei kwenye soko na kukabilian na njaa katika baadhi ya nchi maskini zaidi duniani.
Makubaliano yalifikiwa mnamo mwaka jana ya kuwezesha usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine ambayo yalisimamiwa na Uturuki na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, kabla ya kuusimamisha mkataba huo Urusi alilalamika kwamba vikwazo vya nchi za Magharibi vinazuia usafirishaji wa nafaka kutoka Urusi Kwenda kwenye masoko ya ulimwengu.
Chanzo:DPA