1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaCambodia

Mawaziri wa ulinzi wa Marekani na China wakutana

22 Novemba 2022

Mawaziri wa Ulinzi wa China na Marekani wamekutana kwa mara ya pili Jumanne (22.11.2022) tangu kuanza kwa mwaka huu katika mkutano nchini Cambodia ambao haukutarajiwa kutanzua masuala tete baina ya mataifa hayo mawili

USA Verteidigungsminister Lloyd Austin
Picha: Michael A. McCoy/Pool via AP/picture alliance

Wakati wa mkutano huo uliochukuwa muda wa takriban dakika 90 na ulioelezwa na afisa mmoja wa Marekani kuwa wa tija na utaalamu, Austin, alisisitiza haja ya kuboresha mawasiliano wakati wa mgogoro huku akielezea wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa tabia ya hatari ya ndege za kivita za China.

Austin azungumzia umuhimu wa mazungumzo kuhusu masuala mbali mbali

Katika taarifa baada ya mkutano huo, msemaji wa ikulu ya rais ya Marekani brigadia jenerali Pat Ryder, alisema kuwa wakati wa mkutano huo ambao ni wa pili wa ana kwa ana kati ya Austin na Wei Fenghe mwaka huu, Austin alizungumzia kuhusu umuhimu wa mazungumzo muhimu ya kupunguza athari ya kimkakati na kuimarisha usalama wa utekelezaji.

Austin amuhakikishia Wei kujitolea kwa Marekani kwa sera ya China moja

Ryder ameongeza kuwa Austin alimuhakikishia Wei kuhusu kujitolea kwa rais wa nchi hiyo Joe Biden kwa sera ya China moja. Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa Austin pia alisisitiza upinzani wake kwa mabadiliko ya upande mmoja kwa hali ilivyo, na kuitaka China ijiepushe na vitendo vya kuyumbisha utulivu kuelekea Taiwan.

Taarifa hiyo pia imesema kuwa Austin alizungumzia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kusema Marekani na China, zote zinapinga matumizi ya silaha za nyuklia ama vitisho kuzihusu.

Waziri wa ulinzi wa China - Jenerali Wei FenghePicha: Danial Hakim/AP/picture alliance

Wakati huo huo katika mkutano na wanahabari, msemaji wa wizara ya ulinzi ya China kanali mkuu Tan Kefei, aliyataja mazungumzo ya leo kama hatua madhubuti ya kutekeleza makubaliano muhimu yalioafikiwa kati ya rais wa China Xi Jinping na Biden. Kefei amesema kuwa mkutano huo ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa kurejesha uhusiano kati ya China na Marekani katika njia ya maendeleo bora na thabiti.

Wei asema jukumu la kurekebisha uhusiano kati ya pande hizo mbili ni la Marekani

Lakini taarifa rasmi iliyotolewa na wizara ya ulinzi ya China, imemnukuu Wei kwa kusema kuwa jukumu la hali ilivyosasa katika uhusiano kati ya China na Marekani, liko upande wa Marekani na wala sio China. Wei alisema kuwa suala la Taiwan ni nyeti na ambalo China haitaruhusu muingilio kutoka nje. Wei ameongeza kuwa jeshi la China liko thabiti, lina dhamira, linajiamini na pia lina uwezo wa kulinda umoja wa nchi hiyo.

Taarifa hiyo ya wizara ya ulinzi ya China imeendelea kusema kuwa pande hizo mbili pia zilibadilishana maoni kuhusu bahari ya Kusini ya China, Ukraine na rasi ya Korea bila ya kutoa maelezo.

 

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW