1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa ulinzi wa NATO wajadili mzozo wa Ukraine

Sylvia Mwehozi
15 Juni 2022

Mawaziri wa ulinzi wa jumuiya ya kujihami ya NATO wanakutana mjini Brussels kujadili suala la kutuma silaha nzito Ukraine, wakati nchi hiyo yenyewe ikipuuza muda wa mwisho wa Urusi kujisalimisha mjini Severodonetsk.

NATO-Generalsekretär Stoltenberg
Picha: Yves Herman/REUTERS

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema kuwa kuna "hitaji la haraka" la kuongeza kasi ya usambazaji silaha nchini Ukraine, lakini ameonya kwamba inatumia muda mwingi kwa vikosi vya Ukraine kuzitumia silaha nzito za kisasa. Ameongeza kuwa "Ukraine ipo katika hali ngumu" na hivyo kuna haja ya haraka ya kuongeza hatua.Zelenskiy: Ukraine yakabiliwa na hasara chungu Severodonetsk, Kharkiv

"Washirika wamejitolea kuendelea kutoa zana za kijeshi ambazo Ukraine inahitaji ili kushinda, ikiwa ni pamoja na silaha nzito na mifumo ya masafa marefu. Pia tutajadili jinsi ya kuongeza msaada wa vitendo kwa washirika wengine walio katika hatari, ikiwa ni pamoja na Bosnia Herzegovina, na Georgia."

Mataifa ya Magharibi yamemimina silaha kubwa nchini Ukraine ili kuisaidia kukabiliana na Urusi, lakini Kyiv bado inalalamika kwamba imepokea sehemu ndogo tu ya kile inachokihitaji huku ikitoa wito zaidi wa kupatiwa silaha nzito. Aidha, mkuu huyo wa NATO amesema pia kwamba mkutano wa kilele wa muungano huo wa kijeshi utakaofanyika mjini Madrid baadaye mwezi huu, utapaswa kukubaliana juu ya "mfuko kamili wa usaidizi" kwa Ukraine ili kusaidia vikosi vyake viweze kubadilisha na kuendana na viwango vya silaha za NATO kwa muda mrefu.

Picha kutokea angani katika mji wa SeverodonetskPicha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Naye waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa NATO, na hivyo kumfanya kuwa kiongozi wa kwanza wa Tokyo kufanya hivyo. Kishida amewaeleza waandishi wa habari kwamba "usalama barani Ulaya hauwezi kutenganishwa na usalama ndani ya eneo la Indo-Pasifiki"

Kwa upande wa Kyiv kwenyewe, Ukraine imepuuza muda wa mwisho uliotangazwa na Urusi wa kutaka iusalimishe mji wa mashariki wa Severodonetsk. Urusi ilikuwa imewaeleza wanajeshi wa Ukraine ambao bado wanapambana wakiwa ndani ya kiwanda cha kemikali, kuacha "upinzani usio na msingi na kuweka silaha chini" kuanzia Jumatano asubuhi, wakati ikizidisha mashambulizi ya kudhibiti eneo la mashariki.

Waasi wanaotaka kujitenga wakiungwa mkono na Urusi, wamenukuliwa na shirika la habari la RIA, kwamba mipango iliyotangazwa na Moscow ya kufungua njia ya kiutu kwa ajili ya kuondolewa raia waliokwama kwenye kiwanda cha Azot, iliingiliwa kati na makombora ya Ukraine. Waasi hao walipanga kuwahamisha raia na kuwapeleka katika maeneo wanayodhibiti.

Ukraine inadai kwamba zaidi ya raia 500 wakiwemo watoto 40 wamekwama sambamba na askari ndani ya kiwanda cha kemikali cha Azot, ambako vikosi vyake vimekabiliana kwa wiki kadhaa na mashambulizi ya Urusi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW