1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa viwanda, fedha Afrika Mashariki wakutana Arusha

Veronica Natalis
9 Februari 2024

Mkutano wa 43 wa baraza la mawaziri kutoka sekta za viwanda, biashara, fedha na uwekezaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika mjini Arusha, Tanzania, makao makuu ya jumuiya hiyo siku ya Ijumaa (Februari 9).

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Peter Mathuki.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Peter Mathuki.Picha: Emmanuel Lubega/DW

Mawaziri hao kutoka nchi nane wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamejadili nafasi ya uwekezaji wa sekta binafsi katika sekta za viwanda, biashara na fedha na kikao hicho kimekubaliana kushughulikia vikwazo vya kodi na vile visivyotozwa kodi kwa manufaa ya nchi wanachama.

Jambo lingine lililopewa kipaumbele na kikao hicho ni kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki kuingia makubaliano na jumuiya nyingine za kikanda na mataifa yaliyoendelea ili kukuza biashara.

Soma zaidi: Wakuu wa nchi za EAC wajadili mabadiliko ya tabia nchi

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Exaud Kigahe, alisema wameamua kutumia fursa za biashara ya kimataifa kama jumuiya na sio kama nchi moja moja.

“Kwa mfano tuna EPA au nchi nyingine UK na kadhalika, na sasa tumeona kwamba tuende kama Jumuiya kuliko kwenda nchi kama nchi kwa sababu tumeona kuna manufaa makubwa tukienda kama nchi kuliko kwenda mmoja mmoja. Kama itatokea nchi moja imeingia makubaliano na nchi nyingine, basi tutaona ni kwa namna gani tutashirikiana kama Jumuiya, tukiona kuna manufaa ya kujiunga. Kwa mfano, leo tumejadiliana namna tutakavyojiunga na China, Singapore na nchi nyengine ambazo tunafikiri tunatakiwa kufanya nazo biashara." Alisema.

Sekta binafsi kupewa umuhimu


Nje ya mkutano, naibu waziri huyo wa Tanzania alieleza kuwa mkutano huo wa kisekta uligusia pia suala la biashara huria miongoni mwa nchi wanachama na moja kati mikakati iliyowekwa ni kuondoa vikwazo vya kibiashara.

Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi ambaye ndiye pia raia wa sasa Jumuiya ya Afrika Mashariki.Picha: Tchandrou Nitanga/AFP/Getty Images

Kwa upande wake, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Sudan Kusini, William Anyuon Kuol, pamoja na mambo mengine alisisitiza kwamba ili kuondoa vikwazo vya kibiashara, sekta bianfsi zinatakiwa kupewa nguvu.

Soma zaidi: Somalia karibu Kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki

“Tunazingatia namna ambavyo tunaweza kuzipatia nguvu sekta binafsi katika maeneo ya viwanda na uwekezaji. Tumejadili hayo na tumekubaliana kwamba kila nchi mwanachama wa Jumuiya hii afaidike na suala la sekta binafsi.” Alisema waziri huyo.

Mkutano huo wa mawaziri pia ulizingatia tathimini ya kikanda kuhusu mafanikio ya  eneo moja la forodha, pamoja na ripoti ya hali ya utekelezaji wa mfumo wa kielekroniki wa kufuatilia mizigo.

Maazimo ya kikao hiki yatawafikia wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kufanyiwa maamuzi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW