Mawaziri wa Israel wataka Ukingo wa Magharibi kunyakuliwa
21 Septemba 2025
Mawaziri wawili wa Israel walio na siasa kali za mrengo wa kulia wametoa wito wa kunyakuliwa kwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel kufuatia tangazo la Uingereza, Canada na Australia kulitambua taifa la Palestina. Waziri wa usalama wa taifa Itamar Ben Gvir, amesema leo kwamba tangazo la Uingereza, Canada, na Australia kulitambua taifa la Palestina, linahitaji hatua za haraka za kukabiliana na hali hiyo. Miongoni mwa hatua za haraka alizopendekeza ni kupititishwa kwa mamlaka ya kujitawala huko Yudea na Samaria na kuvunjwa kabisa kwa Mamlaka ya Palestina. Waziri huyo anakusudia kuwasilisha pendekezo la kupitishwa mamlaka ya kujitawala katika mkutano ujao wa baraza la mawaziri. Naye waziri wa fedha Bezalel Smotrich, ambaye mara kadhaa ametaka Ukingo wa Magharibi kunyakuliwa, naye alitoa kauli kama hiyo.