1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wazungumzia kitisho cha mzozo wa chakula

Sylvia Mwehozi
24 Juni 2022

Mawaziri wa mambo ya kigeni, kilimo na maendeleo kutoka kote ulimwenguni wamekusanyika mjini Berlin kwa mkutano wa hali ya usalama wa upatikanaji wa chakula katikati mwa mzozo wa Ukraine.

Deutschland Berlin | Internationale Konferenz zur Ernährungssicherheit
Picha: Florian Gaertner/Photothek/picture alliance

Wawakilishi kutoka nchi takribani 40 zikiwemo zile zilizoathirika zaidi kama Nigeria, Tunisia na Indonesia wanahudhuria mkutano huo uliopewa kichwa cha habari "kuungana kwa ajili ya usalama wa upatikanaji wa chakula", kuelekea mkutano wa kilele wa mataifa 7 yaliyopiga hatua kiviwanda ya G7.

Akizungumza katika mkutano huo waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzidisha juhudi zake katika mapambano ya kukabiliana na hali mbaya ya mzozo wa njaa katika maeneo mengi duniani. Amesema kuwa hali ni mbaya sana huku takribani watu milioni 345 wakiwa katika kitisho cha kukumbwa na ukosefu wa chakula.

"Sio mamia, sio maelfu, ni mamilioni ya watu. Ni wanawake, watoto na wanaume milioni 345 ambao wanatishiwa pakubwa na uhaba wa chakula duniani kote. Ni shida ya chakula ambayo inatukabili kama wimbi la hatari ya maisha. "

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani pia aliishutumu Urusi kwa kutumia njaa "kama silaha" na "kuushika mateka ulimwengu mzima". Ameongeza kuwa hivi sasa kipaumbele ni kutafuta njia za kuaminika za kusafirisha nafaka kutoka Ukraine ili kuzuia mgogoro wa chakula.

Mawaziri wa mamb ya nje wa Marekani na UjerumaniPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Kulingana na waziri wa maendeleo wa Ujerumani, Svenja Schulze watu wapatao milioni 400 ulimwenguni kote wanategemea chakula kutoka Ukraine. Ukiachilia mbali ugavi wake kukwama katika Bahari Nyeusi, lakini kupanda kwa bei za vyakula na nishati vinayaumiza mataifa yaliyo mengi. Urusi imekuwa ikikanusha kuzuia usafirishaji wa meli za vyakula na kuyalaumu mataifa ya Magharibi kwa vikwazo dhidi yake kuwa ndivyo vinachangia mgogoro wa chakula.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amedai kuwa "kuna kitisho halisi" cha njaa mwaka huu na kuwataka mawaziri wanaokutana Berlin kuchukua hatua stahiki za kutuliza masoko ya vyakula na kupunguza hali tete ya kupanda kwa bei. Akizungumza kwa njia ya video, Guterres amesema "vita vya Ukraine vimetokea wakati tayari kuna matatizo yaliyochangiwa kwa miaka mingi na hali ya hewa na janga la COVID-19."

Uturuki imekuwa ikifanya jitihada za kuanza tena kwa usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi na wiki hii ilikubali kuanzisha mazungumzo ya jinsi gani ya kuutatua mzozo huo baada ya kukutana na maafisa wa Urusi.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW