May afikia makubaliano na chama cha DUP
26 Juni 2017Lakini kwa upande mwingine serikali italazimika kuipatia Ireland ya kaskazini fedha za ziada , zaidi ya pauni bilioni moja. hatua hiyo imesababisha mtafaruku katika baadhi ya duru kutokana na historia ya chama hicho ya mawazo yake yaliyosababisha uharibifu na mauaji.
Makubaliano hayo yenye utata na chama cha Northern Irish Democratic Unionist yanakuja baada ya May kulazimika kupoteza wingi wake bungeni katika uchaguzi mapema mwezi huu ambao aliuitisha ili kuimarisha uungwaji wake mkono kwa ajili ya mazungumzo ya nchi hiyo kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya mchakato unaofahamika kama Brexit.
Chini ya masharti ya makubaliano hayo, Ireland ya kaskazini itapokea fedha za ziada pauni bilioni 1.0 sawa na euro bilioni 1.1 kutoka serikali kuu katika muda wa miaka miwili ili chama hicho cha DUP kiweze kukiunga mkono chama cha Conservative cha waziri mkuu May.
Chama cha DUP kimesema kitaiunga mkono serikali katika kila kura ya kuwa na imani na kupitisha bajeti, pamoja na kuunga mkono sheria zinazohusu Brexit.
Kwa kura nyingine zozote bungeni, chama cha DUP, ambacho kina wabunge 10, kimesema uungaji wake mkono utategemea suala na suala.
Makubaliano hayo yalitiwa saini na maafisa waandamizi wa chama cha Conservative na DUP katika ofisi ya waziri mkuu , wakati May pamoja na kiongozi wa DUP, Arlene Foster wakiangalia.
"Kufuatia matokeo ya uchaguzi na uwezo tuliopewa na watu wa Ireland ya kaskazini, tumekuwa katika majadiliano na chama cha Conservative na Unionist juu ya vipi tunaweza kuiunga mkono serikali yenye wingi mdogo ya chama cha Conservative bungeni. Leo tumefikia makubaliano na chama cha Conservative juu ya kuiunga mkono bungeni. Makubaliano yatafanyakazi kuweza kuwezesha kuwa na serikali imara kwa maslahi ya Uingereza katika muda huu muhimu."
Makubaliano yakosolewa
Vyama vya upinzani vimeikosoa haraka hatua hiyo, ambapo kiongozi wa chama cha kiliberali, Liberal Democrats Tim Farron aliyaita, 'makubaliano madogo yasiyo na maana.'
Chama chenye balaa kimerejea, kikisaidiwa na DUP," amesema katika taarifa. Waziri kiongozi wa Wales Carwyn Jones wa chama kikuu cha upinzani cha labour ameliita wazo hilo la muungano "laajabu" na "lisilokubalika" na kusema fedha zilizoahidiwa ni " kifuniko" cha kuiweka serikali iliyodhoofika ya waziri mkuu kuendelea kubakia madarakani.
Tovuti ya habari ya Independent imesema May "analipa gharama kubwa ili kung'ang'ania madarakani".
Chama cha Conservative kina viti 317 katika bunge lenye viti 650 baada ya uchaguzi wa Juni 8 na kinahitaji uungwaji mkono wa chama cha DUP chenye viti 10 ili kiweze kuendelea kutawala.
Makubaliano hayo na chama cha DUP pia yataendelea kuwa yenye utata kwasababu ya upinzani wa chama hicho dhidi ya ndoa za mashoga na utoaji mimba na wasi wasi kwamba yanaweza kuvuruga uwiano tete wa hatua za amani katika Ireland ya kaskazini.
May amesema katika taarifa hata hivyo kwamba "anayakaribisha makubaliano haya ambayo yatawezesha kufanyakazi kwa pamoja kwa maslahi ya Uingereza Uingereza yote."
Chama cha DUP kiliunga mkono Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya lakini kimesisitiza haja ya kuiweka mipaka na jamhuri ya Ireland wazi , na Foster amesema makubaliano hayo yataunga mkono mchakato wa Brexit "ambao unaunga mkono pande zote za Uingereza".
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Josephat Charo