May aihakikishia Ireland kuhusu mpaka
6 Februari 2019Akiwania kupunguza hofu juu ya kurejeshwa kwa vituo vya udhibiti wa mipaka na ukaguzi wa magari, May amesema wakati wa ziara yake mjini Belfast kwamba serikali ya Uingereza ina nia ya dhati ya kuzuwia ujenzi wa kivuko cha upekuzi katika mpaka kati ya Ireland ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya na Ireland ya kaskazini ambayo ni sehemu ya Uingereza baada ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya.
Waziri mkuu amesema alifika mjini Belfast , "kuwahakikishia nia yake ya dhati kukamilisha kujitoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya katika hatua inayohakikisha kwamba hakuna kurejeshwa kwa ukaguzi wa mpakani kati ya Ireland ya kaskazini na Ireland, hali ambayo haitabadilika."
"Pia sitaridhia kuivunja ahadi yangu ya kuilinda Ireland ya kaskazini kama sehemu kamili ya Uingereza. Wakati Halmashauri ya Umoja wa Ulaya ilipopendekeza kuwapo na kituo cha upekuzi, ambacho kinajumuisha kuundwa kwa mpaka wa forodha katika bahari ya Ireland, nilifanikiwa kulipinga hilo. Nilipinga kabisa pendekezo hilo.
Hali hii haitaharibu tu Umoja wa soko la ndani la Uingereza, ambalo ni muhimu sana kwa biashara katika Uingereza, bali pia na hapa Ireland ya kaskazini. Hali hiyo pia itapuuzia wasi wasi wa kweli wa watu wengi juu ya kutengwa na sehemu yote ya Uingereza."
Pia amesisitiza uungaji mkono wa serikali kwa ajili ya makubaliano yanayojulikana kama ya "Ijumaa kuu" , mkataba wa mwaka 1998 ambao kwa kiasi kikubwa ulimaliza miongo kadhaa ya machafuko katika Ireland ya kaskazini yanayofahamika kama "matatizo."
Maneno ya uhakikisho ya May hata hivyo hayakumaliza mkanganyiko uliopo kuhusu mpaka katika suala la Brexit.
Wakati huo huo mawaziri wa Uingereza wamefanya mazungumzo ya siri kuhusiana na mipango ya kuchelewesha Brexit kwa wiki nane, limeripoti gazeti la Telegraph jana jioni.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / rtre
Mhariri: Daniel Gakuba