Mazishi ya pamoja yafanywa Sierra Leone kwa mamia ya maiti
17 Agosti 2017Mazishi ya pamoja ya mamia ya maiti zilizotokana na maporomoko ya matope siku tatu zilizopita yamefanywa leo katika mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown. Aidha kuna hofu kuwa mvua zaidi inayotarajiwa kunyesha huenda ikalemaza juhudi za uokozi wakati ambapo watu 600 bado hawajulikani waliko. Wakati huo huo, serikali imelaumiwa kwa mpango mbovu wa ujenzi katika mji huo.
Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, maiti 150 za watu walioangamia kwenye maporomoko hayo ya matope yaliyotokea siku ya Jumatatu baada ya mvua kubwa iliyonyesha, tayari zimezikwa leo kwenye kaburi la pamoja mjini Freetown.
Haya yanajiri huku serikali ikikabiliwa na ukosoaji mkali wa kutofanya lolote dhidi ya ukataji miti wa kiholela na mpango mbovu wa mjini ambapo baadhi ya wakazi wamejenga chini ya milima na kuondoa mawe au miamba ambayo huzuia matope wakati wa mvua.
Idhaa ya Kiingereza ya DW imezungumza na msemaji wa shirika la Msalaba mwekundu nchini humo Mathew Cochrina na haya ndiyo amesema. "Tunaamini kuwa hadi sasa familia 1,100 zimeathirika, wengi wao hawana makao baada ya nyumba zao kuharibiwa, ni janga kubwa la kibinadamu, na shughuli za kutoa misaada ya kibinadamu zinaendelea. La muhimu zaidi ni kwamba manusura wanahitaji ushauri nasaha."
Imebainika kuwa miongoni mwa walioangamia ni watoto 105. Watu wengine wamesema wamepoteza jamaa zao wote pamoja na mali. Watu 600 bado hawajulikani waliko. Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa takriban watu 3000 wamepoteza makao kufuatia mkasa huo na huenda idadi hiyo ikaongezeka.
Raia pamoja na wataalamu wanaibua maswali ya ni kwa nini serikali ya rais Ernest Bai Koroma haijafanya jambo kudhibiti ujenzi wa nyumba kinyume cha sheria katika mji wa Freetown ambao tayari unakumbwa na msongamano wa wakaazi.
Katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Connaught, miili kadhaa imetapakaa. Maafisa wa Koroma wamesema miili ambayo haijatambuliwa itazikwa katika siku chache zijazo. Aidha Sierra Leone ambayo maelfu ya raia wake waliangamia miaka michache iliyopita kutokana na mripuko wa Ebola, imeomba misaada kutoka kwa jamii ya kimataifa, huku ikiweka mipango maalum ya kuzuia miripuko ya magonjwa kama kipindupindu.
Huku shughuli za uokozi zikiendelea, tabiri za hali ya anga za juma lijalo zinaonesha kuwa mvua itanyesha na hivyo huenda maporomoko zaidi ya matope yakatokea.
Malkia Elizabeth II wa Uingereza ametuma risala za rambirambi kwa Rais Koroma huku akielezea kusikitishwa na mkasa huo.
Mwandishi: John Juma/APE/AFPE
Mhariri: Josephat Charo